Saturday, December 16, 2023

KAMPENI YA 'AFYA CHECK' YAVUTIA VIJANA KUPIMA VVU KWA HIARI MKOANI MBEYA.

Kundi kubwa la vijana Mkoa wa Mbeya limejitokeza kwenye kampeni ya Afya Check kwa ajili ya kupima afya na kujitambua kama wana maambukizi ya virusi vya UKIMWI (VVU).

Kampeni hiyo yenye lengo la kuhamasisha vijana kwenye vyuo vya elimu ya juu 9 na kufikia vijana 4,000 Jijini Mbeya kwa ufadhiri wa Shirika la HJMRI ambayo inaendeshwa kwa makundi mbalimbali mkoani hapa.
Hatua hiyo imefikiwa kufuatia kundi kubwa la vijana kuwa kwenye hatari ya kupata maambukizi ya VVU huku kati ya kundi la watu 10 mmoja hukutwa na maambukizi sambamba na Mkoa kushika nafasi 2 kitaifa kwa kuwa na asilimia 9.3.


Mratibu wa Kampeni hiyo Dkt. Isaac Maro amesema kundi kubwa la vijana liko katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya UKIMWI na ndio maana kampeni hiyo mahususi kama “Jitambue” ililenga kuhamasisha vijana kupima afya zao.

Desemba 16, 2023 wakati akizungumza na wanafunzi wa kituo cha elimu ya Sekondari  cha Sebama na Chuo cha Kilimo Uyole Jijini Mbeya.
“Kundi la vijana liko kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi kutokana na kujamiiana pasipo kutumia kinga ujio wa kampeni hiyo ni kuwaandaa kupima afya na kujitambua ikiwa ni kutekeleza sera ya Taifa ya vijana wa kesho” amesema.

Amesema ili kufikia hatua hiyo wazazi wanapaswa kubeba jukumu la kukaa na vijana kutoa nasaha za umuhimu wa kupima afya bure na kutambua na endapo itabainika kuathirika kuna dawa maalum utolewa ili kuendelea kuishi maisha bora na salama kwa tahadhari kubwa” amesema.

Dkt. Maro amesema kuwa umefika wakati sasa wazazi na walezi kuondoa aibu kwa kukaa na vijana kutoa elimu ya afya ya uzazi na maambukizi ya UKIMWI kutokana na kukua kwa utandawazi kwa lengo la kuokoa kizazi cha sasa na kijacho sambamba na nguvu kazi kwa Taifa.

Pia Dkt. Maro amesema sababu kubwa ya maambukizi kuathiri kundi la vijana ni kutokana na ushiriki wao mkubwa kwenye ngono zisizo salama sambamba na mifumo ya maisha na kukua kwa teknolojia za utandawazi.

Mwanafunzi wa kidato cha sita Shule ya  Sekondari Sebama kituo cha (QT) Saida  Kibona amesema amelazimika kupima afya ili ajitambue na kuweka mipango mizuri ya maisha yake ya baadaye.

Amesema akijua afya yake kutamwezesha kutengeneza kesho yake endapo ikabainika ana maambukizi atalazimika kuishi kwa kuzingatia elimu ya wataalam wa afya.

Amesema kuwa wana kila sababu ya kuishukuru Serikali na wadau wa Shirika HJMRI kwa hatua ya kufadhiri kampeni ya Afya Check ambayo imewafikia kutoa elimu nao kuhamasika kupima kwa hiari.
Mwanafunzi Isakili Edward licha ya wao kuwa na mwamko wa kupima afya bado kuna baadhi yao wanakwepa huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni hofu ya majibu kufuatia kuwepo kwenye mifumo ya tabia za kuwa katika hatari za kupata maambukizi ya UKIMWI.

Kampeni ya Afya Check imezinduliwa Desemba 13 mwaka huu na inatarajiwa kuhitimishwa Desemba 19 katika viwanja vya Ruanda Nzovwe, Jijini Mbeya huku malengo ni kufikia vijana zaidi ya 4,000 katika vyuo vya elimu ya juu tisa zikiwepo shule.

No comments:

Post a Comment