Tuesday, December 26, 2023

MABASI MATANO YAZUILIWA KUENDELEA NA SAFARI MBEYA KUTOKANA NA HITILAFU MBALIMBALI.

Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limeyazuia mabasi matano ya abiria katika Stendi Kuu ya Mabasi Jijini Mbeya kuendelea na safari baada ya kukutwa na changamoto mbalimbali.

Akizungumza mapema leo Desemba 26, 2023 Mwanasheria Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani nchini, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Deus Sokoni baada ya kuendesha zoezi la ukaguzi wa Mabasi, Upimaji wa kilevi kwa madereva na utoaji wa elimu katika Stendi hiyo amesema jumla ya mabasi ya abiria 58 yamekaguliwa ambapo kati ya hayo mabasi matano kutoka kampeni ya TURU BEST, ISAMILO EXPRESS, ARUSHA EXPRESS, MSIGWA na AHMED yalikutwa na hitilafu katika mifumo mbalimbali ikiwemo mfumo wa breki.

“Jeshi la Polisi nchini kwa kushirikiana na mamlaka nyingine kama vile mamlaka ya udhibiti wa usafiri ardhini (LATRA) limepewa mamlaka ya kuzuia chombo cha moto kuendelea na safari pindi linapofanya ukaguzi na kugundua changamoto ikiwemo ubovu na hitilafu katika mifumo ya chombo hicho” amesema Sokoni.

Aidha, Afisa Leseni kutoka mamlaka ya udhibiti wa usafiri ardhini ndugu Amani Masuwe amesema kuwa, wamefanya jitihada mbalimbali kuhakikisha abiria waliokuwa wasafiri na mabasi hayo wanapata usafiri mwingine na wengine kurudishiwa nauli zao ili kufanya utaratibu wa safari kwa siku nyingine.

Naye, Balozi wa usalama barabarani Mkoa wa Mbeya ndugu Yonna Mleka amewataka madereva kujenga utamaduni wa kufanya ukaguzi wa magari yao kabla ya kuanza safari ili kuepuka usumbufu kwao na kwa abiria wanaowasafrisha pamoja na kuepuka madhara mengine wawapo safarini.

Ameongeza kuwa, Mabalozi wa usalama barabarani wataendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi na mamlaka nyingine kutoa elimu kwa abiria kupitia kampeni ya Abiria Paza Sauti (APS), kukemea na kutoa taarifa za madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani na kuhatarisha usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara.

No comments:

Post a Comment