Monday, June 3, 2024

DKT. TULIA ALIPONGEZA JIJI LA MBEYA KUSHIKA NAFASI YA PILI KWA USAFI



Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson amempongeza Mstahiki Meya Jiji la Mbeya, Dourmihomed Issa kwa usimamizi mzuri na kupelekea kushika nafasi ya pili kwa usafi.

Dkt. Tulia ambaye pia ni Mbunge Jimbo la Mbeya mjini amesema hayo Juni Mosi ikiwa ni maadhimisho ya siku ya Mazingira duniani yaliyofanyika katika viwanja vya stendi ya Kabwe Jijini hapa.

"Leo ni siku la Mazingira duniani na sisi tumeadhimisha kwa kufanya usafi nimpongeze jiji letu la Mbeya  chini ya Mstahiki Meya Dourmohamed Issa kwa usimamizi mzuri na kuwezesha kushika nafasi ya pili katika usafi" amesema Dkt. Tulia.

Aidha amesisitiza suala la usafi kwa wananchi Mkoa wa Mbeya iwe ajenda ya kudumu katika kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita.

Kwa upande wake, Mstahiki Meya Jiji la Mbeya Dourmohamed Issa amesema watandelea kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na suala la usafi ili jiji liweze kupanda na kushika nafasi ya kwanza.

No comments:

Post a Comment