Wednesday, June 19, 2024

DC SONGWE AZUIA WACHIMBAJI WADOGO ZAIDI YA 300 KUCHIMBA MADINI

Wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu Kitongoji cha Kampilipili Kijiji cha Mbangala Kata ya Mbangala Wilaya ya Songwe Tarafa ya Kwimba Wilaya ya Songwe Mkoa wa Songwe wamemuomba Waziri wa Madini Anthon Mavunde na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuingilia kati mgogoro katika Kitalu cha Madini kinachomilikiwa na Kampuni ya Denic Mining Limited na Kikundi cha Wachimbaji cha Kampilipili Gold Mine baada ya Mkuu wa Wilaya Songwe Solomon Itunda kuzuia shughuli zote eneo la mgogoro.

Baadhi ya wachimbaji wamepaza sauti zao wakionesha masikitiko yao zaidi wakiituhumu Ofisi ya Madini Mkoa wa Songwe wakidai mchakato wa utoaji leseni umegubikwa na rushwa.

Nelson Kanunga mkazi wa Kampilipili amesema kilio chao ni kunyang’anywa eneo lao kwa dhuluma na maafisa madini kwani wamekuwepo eneo hilo yango mwaka 2011 ambapo zaidi ya watu elfu tatu wameathiriwa na mgogoro huo na kuhatarisha amani hivyo amemuomba Waziri wa Madini na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuingilia kati.

“Mchakato wa utoaji leseni umegubikwa na rushwa kwani walifika ofisi za madini wakitaka kupatiwa eneo hilo lenye hekta 19.5 lakini waliambiwa mtandao unasumbua cha ajabu usiku tulishangazwa kuona ofisi ya madini imetoa leseni 21 kwa Kampuni ya Denic usiku wa manane” alisema Kanuga.

Naye Monica Otieno yeye ni mjasiriamali amesema ana watu kumi na tano wanaomtegemea  kwani wakiondolewa hapo hawana pa kwenda na mara kwa mara wamekuwa wakiondolewa maeneo mbalimbali kama Mlima Mungu na eneo la Lukuvi.

Bertha Nadebayo amesema yeye ni mwamamke kama mchimbaji ameiomba serikali iangalie mgogoro kwa jicho la tatu kwani wanalipa mapato ya serikali na kuchangia huduma za kijamii hivyo kuondoshwa eneo hilo kutavuruga amani.

Kwa upande wake Ayoub Msilikasi amesema alianza uzalishaji mwaka 2011 na shughuli hizo huzifanya kwa mikopo na wamefanya utafiti muda mrefu sanjari na kuchimba kwa kutumia zana duni na wameshangazwa na Afisa madini aliyefahamika kwa jina la Mayala aliyefika eneo lao na kupima akidai eneo limetengwa kwa ajili yao siku chache wakashangazwa na utolewaji wa leseni 21 bila kuwashirikisha.

“Tumechoswa na tabia za maafisa madini wakishirikiana na watu wenye pesa hususani viongozi wa serikali kuwanyanyasa kwa kuwafanya watafiti na baadaye maeneo yao kuchukuliwa na watu wanaodai ni Kampuni”alisema Msilikasi

Amesema Denic ni dalali tu nyuma yake kuna Wachina ambao mitaji yao ni midogo na wanafanya shughuli ambazo zingeweza kufanywa na wachimbaji wadogo kwani sera ya serikali ni kuongeza ajira lakini ofisi ya madini inafisha juhudi za serikali.

Ameenda mbali zaidi kwa kusema serikali imesogeza huduma za umeme eneo hilo ili kuongeza uzalishaji wanapoondoshwa eneo hilo kutaitia hasara kubwa serikali na hawana kwa kwenda hivyo watalilinda eneo lao kwa jasho na damu huku akitishia kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitapoteza kura kwa kuwa wengi wao ni wanachama.

Daniel Kasanga mkazi wa Mabanzi Mwakibete amesema awali alikuwa akifanya vitendo vya uhalifu alipata ushauri hivyo akaacha wizi na kuuza bangi akaanza kuchimba lakini wanapoondoshwa eneo hilo serikali itakuwa inawarudisha kwenye uhalifu.

“Denic kura yake ni moja lakini sisi kura zetu ni zaidi ya mia tano” alisema Kasanga.

Hoja hizo zinaungwa mkono na Goodluck Mungure Mwenyekiti wa Kikundi cha Kampilipil Gold Mine akisema waliitishwa katika kikao na Mkuu wa Wilaya ya Songwe Solomon Itunda na mwakilishi wa Kampuni ya Denic ambapo maridhiano ya awali Mkuu wa Wilaya aliwaruhusu kuendelea na shughuli zao lakini siku chache baadaye wakasitishwa kufanya shughuli zao na kuambiwa kwa sasa eneo hilo linamilikiwa na Denic ambao walipata leseni kutoka serikalini.

Baada ya mazungumzo hayo kushindikana Mei 14, 2024 Mkuu wa Wilaya ya Songwe Solomon Itunda kamati ya usalama Wilaya Songwe ilisimamisha shughuli zote na yeyote ambaye hakuridhishwa na uamuzi huo anaweza kutafuta haki Mahakamani au sehemu nyingine.

Kutokana na uamuzi huo Mungure amesema wanafanya utaratibu wa kupeleka kilio chao kwa Waziri wa Madini Anthony Mavunde ili kupata haki yao kwani wametumia nguvu kubwa katika eneo hilo ambapo amedai mchakato uliotumika kutoa leseni kwa Denic haukufuata utaratibu.

Chone Malembo Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Kimadini Songwe mbali ya kukiri kuwepo kwa mgogoro amesema Kampuni ya Denic Mining Limited inamiliki leseni ndogo (PML) ishirini na moja katika eneo hilo tangu Septemba 26, 2022 ambapo leseni ya utafiti awamu ya kwanza umetolewa Septemba 13, 2022, awamu ya pili septemba 16, 2022 na awamu ya tatu umetolewa Septemba 19, 2022.

Aidha Malembo ametoa wito kwa wachimbaji kufuata utaratibu ili kuweza kumiliki maeneo ya uchimbaji kisheria kwani mezani kwake hakuna maombi yoyote kutoka kwenye Kikundi cha Kampilipili Gold Mine juu ya kuomba eneo la uchimbaji.

Nimemtafuta Meneja wa Kampuni ya Denic kwa njia ya simu amesema eneo hilo linamilikiwa na Kampuni yake hivyo kwa sasa wanahitaji eneo lao liwe wazi kwa kuwa wanalimiliki kihalali na taarifa nyingine za Kampuni ya Denic zinatolewa na msemaji wa Kampuni.

Aidha Mkuu wa Wilaya ya Songwe Solomon Itunda amekiri kusitisha shughuli za uchimbaji eneo la mgogoro huo huo ingawa amekiri Kampuni ya Denic Mining Limited kulimiliki kihalali na suluhu ya mazungumzo kushindikana baada ya kuzikutanisha pande zote zaidi ya mara mbili.

Itunda alisema mazungumzo yaliyofanyika ilikuwa ni kujaribu kutumia busara kuzikutanisha pande mbili zinazokinzana kwa makubaliano ya kufanya kazi kwa ubia hali ambayo wafanyabiashara waliikataa wakidai eneo hilo waachiwe wao.

Hata hivyo Itunda amewashauri wachimbaji kama hawakuridhika na uamuzi waende mahakamani au ngazi nyingine wanayoona inafaa lakini kwa sasa amemwagiza Afisa Madini kuhakikisha suala hilo analisimamia kikamilifu na kama ataona kuna hali ya utulivu basi Kampuni ya Denic itakabidhiwa eneo lake kwa kuwa leseni imetolewa kihalali na serikali.

Busara inapaswa kutumika kuumaliza mgogoro huo kutokana na wachimbaji wadogo kudai wamekuwepo eneo hilo wakichimba dhahabu tangu mwaka 2011.

No comments:

Post a Comment