Monday, June 3, 2024

KAMPUNI YA PCT YAHIMIZA WAKULIMA KUZALISHA PARETO BORA

Kampuni ya Pareto Tanzania(PCT) imehamasisha wakulima kuzalisha pareto iliyobora kwa kuchuma maua yaliyokauka na ubora unaokidhi soko.

Ofisa Pareto PCT, Mussa Malubalo amesema wakati akitoa mafunzo kwa wakulima kupitia Radio ya jinsi ya kuzalisha, kupalilia na kuchuma maua ya pareto iliyo bora.

Malubalo amesema kampuni hiyo licha ya kununua pareto kwa wakulima imekuwa ikitatua changamoto ikiwepo ujenzi wa vikaushio, utoaji wa miche bora na motisha kwa kutambua mchango kwa wanaofanya vizuri.

"Kuna changamoto kwa wakulima kuchuma maua mabichi hali ambayo inasababisha hasara kwa pande zote mbili hivyo wameona ni vyema kutoa elimu katika kuelekea msimu ujao unaanza mwezi June mwaka huu" amesema.

Malubalo amesema kwa msimu huu kampuni imejipanga kununua tani 2,500 kutoka 2,000 katika msimu uliopita ambapo kwa kilo moja wananunua kwa bei ya 3,500 ambayo ni mkombozi kwa wakulima.

Amesema mbali na ununuzi wa tani 2,500 pia wamejipanga kujenge vikaushio 200 tofauti na vilivyopo 321 havikithi mahitaji kulingana na wakulima kuongezeka siku hadi siku.

Naye Mhasibu wa PCT, Gerald Joseph amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wakulima kuzalisha maua bora ya pareto ili kuepuka hasara ambayo inahepukika.

"Kuna baadhi ya wakulima wamekuwa wakifanya mchezo mbaya kwa kuchanganya mapumba na mawe ili kuongeza uzito hali ambayo inasababisha hasara kwa  makampuni" amesema.

Mkulima Gidion Mapunda amesema uwepo wa kampuni hiyo imekuwa mkombozi kwao wameweza kuzalisha kwa ubora na kubadilisha maisha kwa kujenga nyumba bora na maisha mazuri tofauti na miaka ya nyuma.

No comments:

Post a Comment