Jamii imeaswa kutumia muda wao wa ziada kufanya mazoezi ili kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kuwa na afya imara, kuongeza ushirikiano na pia kutumia michezo na vipaji kama sehemu ya kujiongezea kipato.
Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya Dkt. Godlove Mbwaji leo Juni 08, 2024 katika kilele cha Tamasha la michezo na vipaji liliandaliwa na hospitali hiyo na kufanyika kwa wiki nzima katika uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
"Nitoe wito kwa jamii itambue mtaji mkubwa katika maisha yako ni afya yako, hivyo ni vizuri kutumia muda wa ziara tunaoupata kufanya maoezi, kama hauwezi kutenga muda maalumu wa kufanya mazoezi, basi mazoezi yawe sehemu ya mfumo wako wa maisha yako ya kila siku, kwa mfano umeenda kwenye jengo lenye ghorofa kadhaa, usitumie 'lift' kama hauna shida yeyote ya kiafya kwani hiyo itakua fursa yako ya kufanya mazoezi" amesema Dkt. Mbwanji.
Dkt. Mbwanji ameshauri watumishi hao kutumia muda wao wa ziada kuendeleza vipaji walivyonavyo kwani ni fursa nyingine ya kujiongezea kipato. Pia wazazi kuwasaidia watoto wao kuendeleza vipaji vyao ili waweze kufanya vizuri zaidi na kujitengenezea ajira.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya tamasha hilo Dkt. Awesu Mchepange amesema lengo la kuandaa tamasha hilo ni kufahamiana kucheza kwa pamoja, na kuionyesha jamii kwa vitendo namna ya kufanya mazoezi ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
"Tamasha hili limekua fursa ya sisi kama wataalamu wa afya kuonyesha kwa vitendo kwamba suala la mazoezi jamii inapaswa kulitilia mkazo sio tu kuwashauri kuwa wanapaswa kufanya mazoezi, sisi kama wataalamu wa afya tuna jukumu la kuwa mstari wa mbele katika kuonyesha mfano wa kufanya mazoezi" asema Dkt. Mchepange.
Tamasha hilo limehusisha michezo mbalimbali kama mipira wa miguu kwa wanawake na wanaume, kuvuta kamba, pool table, draft, bao la kete, kukimbia, mpira wa wavu, kuimba, maigizo, vichekesho na maonyesho ya mavazi, ambapo michezo yote washiriki wake ni watumishi wa hospitali hiyo.
Washindi wa michezo na vipaji kwenye tamasha hilo wamepata zawadi mbalimbali kama vile fedha taslimu na vikombe.
No comments:
Post a Comment