Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewajengea uwezo waandishi wa Habari Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini namna bora ya kuandika na kuzitumia vizuri kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu.
Meneja wa Mawasiliano Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Boniface Shoo ameeleza kuwa mada kuu zilizowasilishwa na watumishi wa TCRA Makao makuu ni kuhusu maudhui ya mtandaoni na kanuni za utangazaji wakati uchaguzi.
"Duniani kote masuala ya maudhui yameshika kasi na ni muhimu kuhakikisha kwamba tunawawezesha watoa maudhui kuhusu hayo masuala ya kutoa maudhui mtandaoni ili wasitoe vitu ambavyo vinaleta uharibifu katika jamii tukielekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu" amesema Shoo.
Kwa upande wake Mhandisi Baluye Kadaya amewataka Waandishi kuweka mizania sawa pindi wanafanya vipindi na wanasiasa.
Kadaya ametoa rai kwa wamliki wa vyombo vya habari ambao wanaweza kuwa ni wagombea au ana maslahi binafsi kuepuka kufanya upendeleo wa aina yeyote kupitia chombo chake cha habari.
Afisa mawasiliano TCRA Judith Nyange amesema TCRA imebaini kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa maudhui mtandaoni kwa baadhi yao kuweka habari ambazo hazina mzania, maudhui yalikatazwa, kukashfu na kudhalilisha watu.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika mwishoni mwa mwaka huu na uchaguzi Mkuu utafanyika mwaka kesho ambapo hivi sasa zoezi la maboresho ya daftari la wapiga kura linaendelea nchini.
No comments:
Post a Comment