Wednesday, June 5, 2024

AJALI YAUA WATU 13 JIJINI MBEYA



Watu 13 wamefariki Dunia leo Juni 05, 2024 baada ya Lori lililokuwa limebeba shehena ya kokoto kufeli breki na kuparamia magari mengine, bajaji na pikipiki kwenye Mteremko wa Mbembela Jijini Mbeya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya SACP Benjamin Kuzaga amesema ajali hiyo imetokea leo majira ya saa 7:20 mchana katika eneo la Mbembela, Kata ya Nzonvwe Jijini Mbeya katika barabara kuu ya Mbeya - Tunduma, ambapo gari lenye namba za usajili T 979 CVV na likiwa na tela namba T 758 BEU aina ya Scania iliyokuwa ikiendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina la Ross Mwaikambo (40) likitokea Shamwengo likiwa limepakia kokoto, aligongana na gari namba T 167 DLF Toyota Coaster iliyokuwa ikiendeshwa na dereva asiyefahamika kisha kugongana na gari namba T 120 DER Toyota Harrier iliyokuwa ikiendeshwa na Dokta Robert Francis Mtungi (48) Mkazi wa Isyesye.

Kuzaga ameongeza kuwa lori hilo liligonga guta namba yenye namba za usajili MC 660 BCR iliyokuwa ikiendeshwa na dereva asiyefahamika kisha kugonga pikipiki yenye namba MC 889 CKX iliyokuwa ikiendeshwa na dereva asiyefahamika na kusababisha vifo vya watu kumi na tatu (13) kati yao wanawake 5, wanaume 8 na majeruhi kumi na nane (18) kati yao wanawake 4 na wanaume 14 na uharibifu wa vyombo vya moto.


No comments:

Post a Comment