Wednesday, February 14, 2024

JUMATANO YA MAJIVU: TUNAWATAKIA KWARESMA NJEMA.

 

Leo ni Jumatano ya Majivu, siku ambayo ni alama ya kuanza kwa siku 40 za Kwaresma kwa Wakatoliki. Wakatoliki duniani hutumia kipindi hiki kufahamu vizuri kifo na ufufuo wa Yesu kupitia kutubu, kusali, kufunga na kujikana mwenyewe. TUNAWATAKIA MFUNGO MWEMA WA KWARESMA.

DC SONGWE ASIMAMISHA MCHAKATO UTOAJI LESENI MLIMA ELIZABETH.


Mkuu wa Wilaya ya Songwe Mkoa wa Songwe Solomon Itunda amesimamisha mchakato wa utoaji leseni ulioanza kutolewa eneo la Bafex lililopo mlima Elizabeth Kata ya Saza Wilaya ya Songwe Mkoa wa Songwe.

Itunda amechukua hatua hiyo katika mkutano wa wachimbaji wadogo wadogo uliohudhuriwa pia na Mbunge wa Songwe Philip Mulugo,Mwenyekiti wa Halmashauri ya Songwe Abraham Sambila na kamati ya usalama ya Wilaya ya Songwe.

Awali Itunda amepokea malalamiko kutoka kwa viongozi wa wachimbaji Shadrack Mwakyalabwe, Benedict Mwakitonga na Michael Matoke ambao kwa pamoja wao kupitia kikundi cha Songwe Gold Family wameomba leseni thelathini na nne lakini badala yake wakaambiwa kuwa leseni zinazopaswa kulipiwa ni mbuli tu hali iliyozua taharuki kwa wachimbaji ambao walilazimika kufika ofisi ya Madini ili kupata ukweli wa jambo hilo.

POLISI WATAKIWA KUTUNZA MITI KWA FAIDA YA KIZAZI KIJACHO.

 
Polisi Mkoani Mbeya wametakiwa kupanda miti, kuilinda na kuitunza miti hiyo iliyopandwa katika maeneo yao kwa faida ya kizazi kijacho.
 
Wito huo umetolewa leo Februari 14, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ACP Benjamin Kuzaga wakati akiongoza zoezi la upandaji miti kwa Polisi Mkoa wa Mbeya lililofanyika katika uwanja wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoani hapa.

Kuzaga amesema kuwa, zoezi la upandaji miti katika maeneo ya kambi za Polisi, vituo vya Polisi na maeneo mengine ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura.

MRADI LTIP WATATUA MIGOGORO YA MIPAKA SONGWE.

 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Songwe CPA Cecilia Kavishe amesema Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) umetatua migogoro ya kimipaka katika halmashauri hiyo hatua inayowasidia wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji mali kwa amani.

Akizungumza mwishoni mwa wiki Mkwajuni yalipo makao makuu ya halmashauri hiyo, CPA Kavishe amesema wananchi wa wilaya hiyo ni wakulima, wafugaji na wachimbaji wa madini, ujio wa mradi wa LTIP umesaidia kutatua migogoro ya mipaka kati ya wilaya ya Songwe mkoani Songwe na Chunya mkoani Mbeya ambao ulidumu kwa miaka nane tangu kuanzishwa kwa mkoa wa Songwe mwaka 2016.

“Ukiuangalia katika huu mradi hata ulipofika tu siku ya kwanza wakati tunautambulisha kwa wadau, kitu cha kwanza ambacho watu wengi walifurahia kwenye kile kikao ni kwamba tunaenda kutatua migogoro ya ardhi ambayo ilikuwa ya wananchi pamoja na mipaka” amesema CPA Kavishe.

Tuesday, February 13, 2024

'KWA MTOTO ISIISHIE LISHE BORA, LISHE BORA KWA RATIBA SAHIHI'

 

Kaimu Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya Busokelo, David Kittivo akiwa ameshika kitabu cha Mwongozo wa utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Makuzi, Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali waliohudhuria Kikao cha Uzinduzi wa Programu hiyo katika ngazi ya Halmashauri ya Busokelo iliyopo wilayani Rungwe. (Picha na Joachim Nyambo).

Na Joachim Nyambo.

Wataalamu wa masuala ya Afya wana kauli isemayo ujionavyo ni kutokana na vile unavyokula. Hii ina maana anachokula binadamu au kiumbe hai chochote ndicho huufanya mwili wake uonekane vile ulivyo.

Ni kutokana na hali hiyo wataalamu wa masuala ya lishe wanasisitiza pia umuhimu wa lishe bora kwa watoto kuanzia wakiwa kwenye matumbo ya mama zao, baada ya kuzaliwa na kadiri wanavyoendelea kukua hadi kufikia utu uzima na hadi uzeeni.

 

Afisa Maendeleo ya Jamiii Mkoa wa Mbeya, Elukaga Mwalukasa (kushoto) akimkabidhi Kaimu Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya Busokelo, David Kittivo kitabu cha Mwongozo wa utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Makuzi, Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) baada ya uzinduzi wa Programu hiyo kwenye ngazi ya halmashauri.(Picha na Joachim Nyambo).

Wataalamu wa Afya wanaeleza kuwa Lishe bora kwa mtoto ni sehemu ya mambo muhimu matano yanayowezesha ukuaji stahiki wake. Yaani Lishe inaungana na mambo mengine manne ambayo ni pamoja na Malezi yenye muitikio, Afya bora, Ulinzi na Usalama na Ujifunzaji wa awali.

"MADIWANI TUMIKENI KUDHIBITI UBADHIRIFU WA FEDHA ZA MIRADI YA MAENDELEO" DORMOHAMED ISSA MSTAHIKI MEYA WA JIJI LA MBEYA.


Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Dormohamed Issa amewataka Madiwani kuanza ufuatiliaji wa fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa lengo la kudhibiti ubadhirifu wa kodi za watanzania.

Issa amesema Leo Jumanne, Februari 13, 2024 wakati akifunga kikao cha baraza la madiwani cha kawaida cha kupendekeza bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 ya zaidi ya Sh 91 bilioni.

Issa amesema  umefika wakati madiwani katika maeneo yao kuisadia Serikali kufuatia fedha za miradi ya maendeleo ya wananchi hatua kwa hatua sambamba na  kutoa taarifa kwa ambayo wataitilia mashaka.

“Madiwani Serikali inashusha fedha nyingi sana za miradi kwenye kata zenu sasa fuatilieni hatua kwa hatua kubaini uhalisia wa matumizi kwani tumepata fedha nyingi za miradi, sambamba na kumshukuru Mbunge, Dkt. Tulia Ackson kwani amekuwa kiungo kikubwa kwa hatua za maendeleo tuliyopiga kama Jiji” amesema.

Monday, February 12, 2024

AFISA MTENDAJI WA KATA AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUOMBA RUSHWA YA LAKI MBILI.

Afisa Mtendaji Kata ya Lusungo, Edestus Clemence Ndunguru amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kyela kwa shtaka la kuomba na kupokea Rushwa ya Tsh. 200,000 ili amsaidie Mwananchi kuongea na Askari Polisi waweze kumpa dhamana katika Kituo cha Ipinda.

Kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na 11 ya Mwaka 2007. Mshtakiwa alipelekwa Mahabusu kwa kutokutimiza masharti ya Dhamana huku Kesi ikiahirishwa hadi Februari 20, 2024.

POLISI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA UWELEDI NA KUMTANGULIZA MUNGU.

Maafisa wa Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na kumtanguliza Mungu ili kufikia malengo ya Jeshi na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Polisi SACP Robert Mkisi amewaasa leo Februari 12, 2024 alipotembelea Mkoa wa Mbeya na kukutana na mwenyeji wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ACP Benjamin Kuzaga na Maafisa wengine na kufanya mazungumzo.

Mkisi alipata kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Jeshi la Polisi ikiwemo Mkuu wa Shule ya Polisi Tanzania zamani CCP, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kigoma.

 

Kamishna Mkisi ameendelea kuwajengea uwezo wa utendaji kazi Maafisa, Wakaguzi na Askari Polisi katika nyanja mbalimbali ili kuleta uweledi na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Kipolisi.

MRADI WA LTIP TUMAINI JIPYA LA KUINUA UCHUMI WA WILAYA YA MAKETE

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) ni tumaini jipya la kuwainua kiuchumi wananchi wa wilaya ya Makete kwa ardhi yao kupangwa, kupimwa na kupata hati miliki ya ardhi ili kuendesha maisha yao ya kila siku kwa tija.

Lengo la kutekeleza mradi huo katika katika Halmashauri ya Makete na kusimamiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ni kuboresha usalama wa milki za ardhi kwa kutoa hati miliki za ardhi za kimila kwa wananchi wa halmashauri hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi ya Halmashauri ya wilaya ya Makete mkoani Njombe Bw. William Makufwe hivi karibuni wakati anatoa tathmini ya utekelezaji wa mradi huo wilayani hapo.

Friday, February 9, 2024

DC MALISA AWAKUMBUSHA MSD KUSIMAMIA VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA KUKUSANYA MAPATO.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa imeitaka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) Nyanda za Juu Kusini  kuvisimamia vituo vya kutoa huduma za afya katika maeneo yao ili viweze kukusanya mapato ya kutosha yatokanayo na uchangiaji wa huduma za afya ikiwepo ununuzi wa bidhaa.

Malisa amesema leo Ijumaa Februari 9, 2024 wakati akifungua mkutano wa wadau wa afya na watoa huduma mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Juma Homera.

Amesema Bohari ya Dawa Kanda ya Mbeya inatekeleza majukumu mawili ya kutunza na kusambaza bidhaa kwenye halmashauri 17 zenye vituo vya afya vya kutolea huduma za ya 884 katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Makete Mkoa wa Njombe.

Thursday, February 8, 2024

CHAMA CHA MAPINDUZI KUJA NA MKAKATI MAALUMU WA KULIPENDEZESHA JIJI LA MBEYA.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amesema atazungumza na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dkt. Tulia Ackson ambaye pia ni Rais wa Mabunge Duniani na Spika wa Bunge ili kuja mkakati wa kuzitengeneza barabara za mitaani, ili kulipendezesha jiji hilo.

Makonda ametoa kauli hiyo katika Mkutano wa hadhara uliofanyika jana Februari 7, 2024 katika Uwanja wa Ruanda Nzovwe, Jijini Mbeya mara baada ya kutoridhishwa na majibu ya Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) mkoani humo, Albert Kindole kuhusu ujenzi wa barabara za mitaa ya Jiji hilo.

"Nitafanya mpango wa kuonana na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dkt. Tulia, pia tutawasiliana na Waziri wa Tamisemi (Mohamed Mchangerwa) ili kuweka mkakati maalumu wa kulifanya Mbeya liwe jiji kweli kweli," amesema Makonda.

Awali akijibu swali la Makonda kuhusu mikakati ya ujenzi wa barabara, Meneja wa TARURA Kindole amesema barabara nyingi (takribani kilomita 18) za Jiji la Mbeya bajeti yake imeshatoka na wakandarasi wapo kazini, jambo lililoibua kelele za wananchi waliokuwa katika mkutano huo kuashiria bosi huyo haelezi ukweli.

Wednesday, February 7, 2024

SUMA JKT YAPATA TENDA YA UZOAJI TAKA KATA TANO ZA JIJI LA MBEYA

Halmashauri ya Jiji la Mbeya imekabidhiwa magari 11 na Kampuni tanzu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Suma JKT kwa ajili ya kuanza mkataba wa  uondoshwaji wa taka katika kata tano.

Kampuni hiyo imepata  zabuni kati ya makampuni 16 yaliyojitokeza, huku ikieleza malengo yake ni  kuhakikisha Halmashauri ya Jiji la Mbeya inarejea katika nafasi ya kwanza kwa usafi katika Majiji kutoka nafasi ya mwisho.

Akizungumza na waandishi wa juzi baada ya kukabidhi magari hayo, Mkurugenzi mwendeshaji  kampuni ya usafi, Kepteni Rosemary Katani amesema wamejipanga kurejesha  hali ya usafi kwa Jiji la Mbeya.

“Tumejipanga kuhakikisha Jiji linarejea kwenye nafasi nzuri katika suala la usafi, kwa sasa tumekuja na vifaa vya kisasa na nguvu kazi kwa vijana 50 watakaofanya kazi usiku na mchana taka zote zinaondolewa kwa muda mfupi” amesema Nchimbi.

Friday, February 2, 2024

DC WA SONGWE ATEMBELEA WAATHIRIKA WA MAFURIKO KIJIJI CHA NDANGA, AAGIZA WAHAME.

Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Solomon Itunda ameagiza wananchi wa Kijiji cha Ndanga Kata ya Mbuyuni ambao nyumba zao zimeathiriwa na maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha waondoke katika eneo huku akiutaka uongozi wa Kata hiyo kufanya tathimini na kusimamia zoezi la wananchi hao kuhama.

Itunda ametoa maagizo hayo baada ya kutembelea eneo hilo ambapo, zaidi ya kaya 100 zimaathirika baada ya maji kujaa kwenye makazi yao na kuharibu nyumba na vitu mbalimbali.

“Baada ya kupata taarifa ya mafuriko kupitia diwani tumeamua kuja kujionea wenyewe. Viongozi tuna jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa wananchi wanaishi mahali salama lakini tuna jukumu kubwa kuwafariji wanapokutana na changamoto hii ya mafuriko’’ amesema Mkuu huyo wa Wilaya.