Vituo 50 vya kuchaji magari ya umeme kusimikwa katika mikoa yote nchini, serikali yapanga kununua magari ya umeme na kuhamasisha matumizi ya gesi asilia
Na Sanula Athanas aliyekuwa Dodoma
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, akiwa pamoja na viongozi wengine, akiweka jiwe la msingi wakati wa uzinduzi wa kituo cha kuchajia vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme katika Ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) jijini Dodoma, Juni 11 mwaka huu. PICHA: SANULA ATHANAS
KILA siku, Juma Mwinuka (29) huamka alfajiri na kuanza kazi yake ya kubeba abiria kwa bajaj katika eneo la Kimara Golani, jijini Dar es Salaam.
Kwa miaka mingi alikuwa akitumia bajaj inayotumia petroli, jambo lililomlazimu kutumia kati ya Sh. 20,000 na 25,000 kwa siku kununua mafuta.
Lakini leo maisha yake yamebadilika. Akiwa ameketi katika bajaj yake ya umeme, Mwinuka anasema ameshuhudia tofauti kubwa kati ya teknolojia ya zamani na mpya.
“Nilikuwa natumia Sh. 20,000 hadi 25,000 kwa siku kununua petroli. Sasa nachaji bajaj yangu kwa gharama isiyozidi Sh. 8,000 kwa siku,” anasema huku akitabasamu.
Kwa mahesabu yake, fedha ambazo zamani zilikuwa zinaishia vituoni kununua mafuta sasa zimeanza kubaki mfukoni mwake kama faida.
“Matengenezo ya bajaj yamepungua na faida imeongezeka. Kelele zimepungua na hata abiria wengi wanaipenda hii ya umeme kwa sababu ni tulivu na haina moshi,” anasema.
Moja ya bajaj zinazotumia umeme kama ilivyonaswa na kamera yetu Juni 29 mwaka huu, Kitunda jijini Ilala. Tanzania iko katika harakati za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ili kukabiliana na uchafuzi wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi. PICHA: SANULA ATHANAS
Ushuhuda wa kijana Mwinuka unaakisi mwanzo wa sura mpya katika sekta ya uchukuzi nchini, ambapo matumizi ya umeme yanaanza kuchukua nafasi ya mafuta kama chanzo kikuu cha nishati kwa vyombo vya usafiri.
Ni mapinduzi yanayokuja wakati dunia ikikabiliwa na changamoto za kupanda kwa bei za mafuta, mabadiliko ya tabianchi na haja ya kutafuta vyanzo vya nishati safi na vya gharama nafuu.
ENZI MPYA
Kwa Tanzania, safari hiyo imeanza rasmi. Kwa miongo mingi, magari madogo, mabasi, malori, pikipiki na bajaj nchini vimetegemea petroli na dizeli.
Hali hiyo imeifanya Tanzania kutumia fedha nyingi za kigeni kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi huku uchafuzi wa mazingira ukiendelea kuongezeka.
Hata hivyo, uzinduzi wa vituo vya kuchaji vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme uliofanywa na serikali kupitia Wizara ya Nishati Juni 11 mwaka huu jijini Dodoma, ni kiashirio cha mwanzo wa zama mpya katika sekta ya uchukuzi.
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, anasema changamoto za mara kwa mara za bei za mafuta duniani zimeonesha umuhimu wa kuharakisha matumizi ya nishati mbadala katika sekta ya uchukuzi.
Anasema Tanzania haiwezi kuendelea kutegemea mafuta pekee wakati ina utajiri mkubwa wa vyanzo vya nishati vinavyoweza kuzalisha umeme wa kutosha kwa matumizi ya wananchi na viwanda.
“Ni wakati sasa wa kuanza kufanya mageuzi katika sekta ya uchukuzi kwa kuhamia kwenye matumizi ya magari yanayotumia umeme.
“Hii itasaidia kupunguza utegemezi wa mafuta na kulinda uchumi dhidi ya misukosuko ya bei katika soko la dunia,” anasema.
Kauli hiyo inakuja wakati ambapo kila ongezeko la bei ya mafuta duniani limekuwa likiongeza gharama za usafirishaji, uzalishaji wa bidhaa na maisha ya wananchi kwa ujumla.
Kama ilivyodokezwa awali na dereva bajaj Mwinuka, Waziri Ndejembi anasema magari ya umeme yana gharama ndogo za uendeshaji na matengenezo, jambo linaloweza kusaidia kupunguza gharama za usafiri kwa wananchi na wafanyabiashara.
VITUO 50 NCHINI
Moja ya changamoto kubwa ambazo dereva Mwinuka anataja katika matumizi ya magari ya umeme ni upatikanaji miundombinu ya kuchaji.
Serikali imeanza kukabiliana na changamoto hiyo. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, anasema mashine 50 za kisasa za kuchaji magari ya umeme zimepatikana kupitia ushirikiano kati ya TANESCO na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
“Mashine hizo zitasimikwa katika ofisi za TANESCO za mikoa yote nchini. Hii itawawezesha watumiaji wa magari ya umeme kufanya safari zao kwa uhakika zaidi,” anasema.
Twange anasema mpango huo unatarajiwa kuondoa hofu ya watumiaji kuhusu upatikanaji huduma za kuchaji na hivyo kuongeza kasi ya matumizi ya magari ya umeme nchini.
Magari ya umeme na vyombo vingine vya usafiri vinavyotumia nishati hiyo vikioneshwa wakati wa uzinduzi wa kituo cha kuchajia (EV Charging Station) cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) jijini Dodoma, tarehe 11 Juni 2026. Hatua hii ni sehemu ya mikakati ya serikali ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi. PICHA: SANULA ATHANAS
Mei 12, 2023, gazeti The Citizen lilimnukuu Mtaalamu wa Miradi wa UNDP Tanzania, Dk. Abbas Kitogo, akisema Tanzania inaongoza Afrika Mashariki katika matumizi ya magari na bajaj zinatotumia umeme, lakini kuna changamoto nyingi za kisera, kiteknolojia, kiuwekezaji, miundombinu na uelewa mdogo.
“Hivyo, kazi kubwa inatakiwa kufanyika kupunguza changamoto hizi. Tunaweza kusema bado Tanzania iko katika hatua za mwanzo katika matumizi ya teknolojia hii,” Dk. Kitogo alisema.
Katika kipindi hicho, ripoti iitwayo E-Mobility Alliance iliyotolewa Machi 2023, ilionesha kuwa idadi ya vyombo vya usafiri vitumiavyo umeme nchini ilikuwa takriban 5,000, lakini uchache wa vyombo hivyo ulitokana na kodi kubwa, uelewa mdogo, mafundi wachache, watu kutokuwa karibu na umeme, pamoja na kutokuwapo sera za wazi kuhusu teknolojia hiyo.
Katika kutatua changamoto hizo, Juni 11 mwaka huu, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar alitangaza bungeni jijini Dodoma kuwa serikali imeamua kupunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 10 kwa baadhi ya magari yanayotumia umeme, hatua inayolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi na mbadala nchini.
Alisema uamuzi ni sehemu ya hatua za kikodi zinazolenga kuchochea matumizi ya teknolojia za nishati safi katika usafirishaji.
Vilevile, alisema serikali imeamua kutoa unafuu wa ushuru wa forodha kwenye betri za umeme za umeme zinazotumiwa na wazalishaji au waunganishaji wa magari, bajaj na pikipiki za umeme.
Kwa mujibu wa Waziri Omar, utekelezaji hatua hizo utaanza rasmi Julai Mosi 2026, yaani katika mwaka ujao wa fedha.
UZALISHAJI UMEME
Mapinduzi ya usafiri wa umeme hayawezi kufanikiwa bila kuwa na umeme wa kutosha, wa uhakika na unaofika kila kona ya nchi.
Kwa kutambua hilo, serikali imeendelea kuwekeza mabilioni ya shilingi katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme.
Waziri Ndejembi anasema hadi Machi 2026 uwezo wa kuzalisha umeme nchini ulifikia megawati 4,522.54 kutoka megawati 4,031.71 mwaka uliopita, sawa na ongezeko la asilimia 12.17.
Ongezeko hilo limetokana na kukamilika kwa miradi mbalimbali ya uzalishaji umeme ukiwamo mradi wa umeme wa jua wa Kishapu mkoani Shinyanga wenye uwezo wa kuzalisha megawati 50.
Tanzania pia inaendelea kunufaika na vyanzo mbalimbali vya nishati vikiwamo maji, gesi asilia, jua, upepo, jotoardhi, tungamotaka na urani.
Utajiri huo wa rasilimali unaifanya Tanzania kuwa na nafasi ya kipekee ya kuwa kitovu cha nishati katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Sambamba na kuongeza uzalishaji, Waziri Ndejembi anasema serikali imeendelea kupanua mtandao wa usafirishaji na usambazaji umeme nchini.
“Hadi Machi 2026, urefu wa njia za kusafirisha umeme ulikuwa umefikia kilomita 8,500.38 huku mtandao wa usambazaji ukifikia kilomita 240,229.56.
“Katika kipindi hicho, kiwango cha upatikanaji umeme nchini kiliongezeka kutoka asilimia 78.4 mwaka 2020 hadi asilimia 85.5. Idadi ya wananchi waliounganishiwa umeme pia imeongezeka kutoka asilimia 37.7 hadi asilimia 52.1.
“Serikali imeweka lengo la kuunganisha wateja wapya milioni 8.3 ifikapo mwaka 2030 ili kufikia asilimia 75 ya wananchi wote kuunganishiwa umeme,” Waziri Ndejembi anasema.
TRILIONI 1.416/-
Katika kuimarisha upatikanaji umeme vijijini, Waziri Ndejembi anasema serikali imeanza kutekeleza mradi mkubwa wa kupeleka umeme katika vitongoji 9,009 kwa gharama ya Sh. trilioni 1.416.
Anasema mradi huo unatarajiwa kuongeza shughuli za uzalishaji mali, kuboresha huduma za jamii na kupanua matumizi ya umeme katika maeneo ya vijijini.
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi. Picha na Wizara ya Nishati
Waziri huyo anafafanua kuwa ongezeko la matumizi ya umeme vijijini ni msingi muhimu wa kuandaa soko la baadaye la magari ya umeme, pikipiki za umeme na vifaa vingine vinavyotumia nishati safi.
AJENDA YA SADC
Mwelekeo huo unaendana na malengo ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ambayo Tanzania ni mwanachama mwanzilishi.
Kupitia Itifaki ya Nishati iliyoridhiwa na nchi wanachama mwaka 1996, SADC inasisitiza matumizi ya nishati safi, usalama wa nishati, kuimarisha miundombinu ya umeme na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hatua za Tanzania zinaifanya kuwa miongoni mwa nchi zinazoanza kuweka msingi wa uchumi wa kijani unaotegemea nishati safi badala ya mafuta yanayoagizwa kutoka nje.
Ziara ya juma moja (Juni 21-27 mwaka huu) ya viongozi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Zambia waliokuja kujifunza uzoefu wa Tanzania katika utekelezaji miradi ya umeme vijijini ni uthibitisho wa mafanikio yanayopatikana nchini.
Juni 24 mwaka huu, Mtendaji Mkuu wa REA Zambia, Alex Mbumba akiwa ziarani mkoani Dodoma, alisema: “Tumekuja Tanzania kujifunza na kujionea namna miradi ya umeme vijijini inavyotekelezwa baada ya mafanikio makubwa yaliyofikiwa ya kufikisha umeme kwenye vijiji vyote.”
Meneja wa Usimamizi wa Miradi ya Kupeleka Umeme Vijijini kutoka REA Tanzania, Deogratius Nagu, anasema ujio wa ugeni huo kutoka REA Zambia ni ishara ya kutambuliwa kwa mafanikio ya Tanzania katika kupeleka huduma ya umeme kwa wananchi walioko vijijini.
“Tanzania ni moja ya nchi chache barani Afrika zilizofanikiwa kufikisha umeme katika vijiji vyake vyote, hivyo wenzetu wa Zambia wameona waje wajifunze ni kwa namna gani tumefanikiwa kutekeleza miradi yetu na kufikia mafanikio hayo,” anasema.
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeitambua sekta ya nishati kuwa mhimili mkuu wa mageuzi ya kiuchumi na kijamii.
Dira hiyo inalenga kujenga mfumo wa nishati safi, wa gharama nafuu, wa kuaminika na unaostahimili changamoto za siku zijazo.




No comments:
Post a Comment