Thursday, May 16, 2024

"WAANDISHI WA HABARI TUMIENI WELEDI KWENYE KAZI ZENU" DC MALISA


Serikali mkoani Mbeya imesema iko tayari kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari ili kuandika habari zenye kugusa jamii ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu na pia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Mbeya Beno Malisa wakati akimuwakilisha Mkuu mkoa wa Mbeya Juma Homera kwenye maadhimisho ya Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani ambapo kwa ngazi ya mkoa yamefanyika Mei 15, 2024 katika ukumbi wa Coffee Gadern jijini Mbeya.


Malisa amewataka waandishi wa habari mkoani hapa kutumia weledi na taaluma yao vizuri katika shughuli zao za kila siku. Pia amewataka waandishi kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazojitokeza kwenye maeneo yao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya SACP Benjamin Kuzaga amesema wanahabari wamekuwa watu muhimu kwenye jamii kutokana na mchango mkubwa wa kuhabarisha umma huku akiwataka kuendelea kufichua vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na watu wasio wema.


Awali akiwasilisha risala ya waandishi wa habari kwa mgeni rasmi, Katibu Mkuu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya Elizabeth Nyivambe amesema uwepo wa hiyo umesababisha taaluma ya habari kukua sambamba na kuongezeka kwa ufikishwaji wa taarifa kwa jamii.

Maadhimisho hayo yamekwenda na kauli mbiu inayosema "Uandishi wa habari na changamoto za mabadiliko ya tabianchi".

 

No comments:

Post a Comment