Thursday, May 30, 2024

DC MALISA AAGIZA VIONGOZI ISYESYE KUFANYA MKUTANO WA WANANCHI

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa ameagiza viongozi wa Kata ya Isyesye Jijini hapa kuitisha mkutano wa wananchi kujadili changamoto mbalimbali na kuzitatua.

Malisa amesema jana Mei 29, 2024 kwenye mkutano wake wa kusikiliza kero za wananchi katika kata ya Isyesye jijini hapa ikiwa ni mkakati wake wa kupita kata kwa kata mtaa kwa mtaa sambamba na kuanzisha kliniki ya ardhi.

Miongoni mwa kero alizosikiliza ni pamoja ukosefu wa huduma ya maji,wizi wa mita za maji migogoro ya ardhi katika eneo la shule urasimishaji wa maeneo na fidia.


"Viongozi itisheni mkutano wa wananchi mjadilili na kusikiliza kero zao nimesikia hapa kero mbalimbali sambamba na hilo la wanafunzi kulishwa chakula chenye wadudu" amesema.

Aidha Malisa ameagiza uongozi wa Halmashauri ya Jiji kufanya uchunguzi kwenye shule ya sekondari Isyesye inayomilikiwa na serikali kubaini  malalamiko ya watoto kulishwa chakula chenye wadudu.

"Jamani tunaona Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan anavyoleta miradi mbalimbali ya maendeleo kama afya, elimu, barabara ni vyema kumuunga mkono sambamba na Mbunge wenu Dkt. Tulia Ackson.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Jiji aliyemuwakilisha Mkurugenzi, Dkt Yesaya Mwasubila amesema watafuatilia changamoto ya chakula kilicho lalamikiwa na wazazi, pia ameweka bayana serikali kutoa Tsh 500 milioni ujenzi wa kituo cha afya.

Diwani wa kata ya Isyesye, Ibrahim Mwampwani ameomba serikali kuharakisha kusogeza huduma za afya ili kuwaondoa wananchi na hadha ya kutembea umbali mrefu kifuata huduma hususani kwa wajawazito.

No comments:

Post a Comment