Friday, May 24, 2024

MASACHE AOMBA SERIKALI KUBORESHA VIWANJA VYA MICHEZO MBEYA

Mbunge wa Jimbo la Lupa Masache Kasaka ameiomba Serikali kuboresha uwanja wa Sokoine uliopo Jijini Mbeya na pia kukamilishwa kwa ujenzi wa uwanja unapatikana katika kata ya Mbugani wilayani Chunya.

Masache ameyasema hayo Bunge Jijini Dodoma wakati akichangia hotuba ya makadirio ya bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo iliyowasilishwa na Waziri mwenye dhamana Dkt. Damas Ndumbaro.

 "Mimi natoka Chunya, sisi tumepata bahati ya kupandisha timu ya ligi kuu msimu ujao KenGold FC, Mbeya sasa tuna timu mbili za ligi kuu Tanzania Prisons na KenGold FC, na timu moja ya daraja la kwanza Mbeya City, tunaiomba Serikali iboreshe uwanja wa Sokoine ili uwe bora zaidi, lakini pia sisi Chunya tulianza ujenzi wa uwanja wetu wa michezo, tunaiomba Serikali itupe fedha tukamilishe ule uwanja ili wanachunya waone sasa umuhimu wa kuwa na timu ya ligi kuu" amesema Masache.

Mbali na hayo Masache ameongeza kuwa fursa mbalimbali zitaendelea kufunguka wilayani Chunya endapo uwanja ukikamilika kwa wakati na timu ya KenGold FC kuutumia katika michezo yao ya nyumbani.

No comments:

Post a Comment