Sunday, April 14, 2024

MLIMA KAWETELE WAMEGUKA NA TOPE KUFUNIKA MAKAZI YA WATU

Watu kadhaa wanaripotiwa kukosa makazi mkoani Mbeya kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na kusababisha kumeguka kwa Mlima Kawetele na tope la mlima huo kufunika makazi ya watu leo Aprili 14, 2024.

Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoani Mbeya imetembelea Mlima Kawetele uliopolomoka alfajiri ya leo na kusababisha kufukiwa kwa nyumba 20, ng’ombe wanne na kuharibika kwa miundombinu ya Shule ya Mary's iliyopo Mtaa wa Gombe, Kata ya Itezi, Jiji la Mbeya.

Akizungumza baada kuwasili eneo hilo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambae pia ni Mwenyekiti wa kamati hiyo Juma Homera amekanusha uvumi unaozagaa mtandaoni ukidai kuwa kuna maafa katika tukio hilo ambapo amesema zaidi ya hivyo vilivyotajwa hakuna madhara mengine wala maafa kama inavyoripotiwa na baadh ya watu.

Homera ameiagiza Halmashauri ya Jiji la Mbeya kufanya tathmini juu ya waathirika hasa wale waliokosa malazi wahakikishe wanapatiwa mahali pa kujihifadhi wakati huu ambao serikali inaendelea kupambana kuhakikisha hali inakuwa sawa katika maeneo hayo.

Pia amekiagiza kitengo cha Ardhi cha Halmashauri hiyo kuacha kuwapimia wananchi viwanja eneo lenye changamoto hasa ya mkondo wa maji ili kuepuka matatizo kama hayo ambayo yangeweza kuzuilika.

Tukio hilo limetokea alfajiri ya kuamkia leo kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini. Hivi karibuni mikoa ya Arusha na Lindi pia imekumbwa na mafuriko na kusababisha vifo na uharibifu wa mali na miundombinu mbalimbali.

 

No comments:

Post a Comment