Tuesday, April 9, 2024

MTOTO WA SIKU 27 AFANYIWA UPASUAJI KICHWANI NA KUONDOLEWA UVIMBE WENYE KILOGRAMU 1.8

Ikiwa ni siku ya kwanza ya kambi maalumu ya Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya fahamu kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari Bingwa wa upasuaji wa mifumo ya fahamu, ubongo na uti wa Mgongo (Neurosurgeons) TNS, jana Aprili 08, 2024 wameanza rasmi zoezi la upasuaji kwa wagonjwa 3 waliofika hospitalini hapo wakiwa na matatizo tofauti.

Katika moja ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji, madaktari Bingwa hao wamefanikiwa kumfanyia upasuaji mtoto wa siku 27 na kuondoa uvimbe wenye kilogramu 1.8 aliozaliwa nao sehemu ya nyuma ya kichwa chake upasujia uliochukua takribani saa moja kukamilika.


Mbali na upasuaji huo wataalam hao pia wamefanikiwa kuwafanyia upasuaji wagonjwa wawili mmoja akiwa ni mtoto mwenye umri miezi 9 aliyekuwa na tatizo la mgongo wazi na kufanikiwa kufunikwa eneo hilo kupitia upasuaji uliofanyika kwa muda wa saa moja, na mgonjwa mwingine ni mtu mzima mwenye umri wa miaka 39 aliyevunjika pingili ya katikati ya uti wa mgongo baada ya kupata ajali na madaktari hao waliweza kufanikisha upasuaji huo uliochukua muda masaa mawili.

Kambi hiyo ya upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya fahamu inaendelea kwa muda wa siku tano ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, ikilenga kutoa huduma hiyo kwa wananchi wa Nyanda za Juu Kusini ikiwemo mikoa ya jirani na Mbeya.

No comments:

Post a Comment