Tuesday, April 2, 2024

MADAKTARI BINGWA KUWEKA KAMBI YA SIKU NNE HOSPITALI YA RUFAA KANDA MBEYA

Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya (MZRH) kwa kushirikiana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya wameandaa kambi ya kutoa huduma upasuaji kwa watu wenye magonjwa mbalimbali.

Kambi hiyo itahudumiwa kwa ushirikiano wa madaktari bingwa wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambao ni wataalamu wa magonjwa ya ubongo, mishipa ya fahamu, saratani pamoja na magonjwa ya mifupa.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji amesema kambi hiyo itachukua siku nne kuanzia Aprili 8 hadi Aprili 12, 2024 na baada ya muda huo kuisha huduma hizo zitaendelea kutolewa katika hospitali hiyo.

Dkt. Mbwanji ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Mbeya na mikoa jirani kutumia fursa hiyo kwa kuwa huduma hizo zitatolewa kwa gharama nafuu zaidi jambo ambalo hapo awali ililazimika mgonjwa kupelekwa Muhimbili kwa gharama kubwa.

"Wananchi watumie fursa hii kufika hospitalini hapa kwasababu tutakua na madaktari bingwa na wabobezi kutoka sehemu mbalimbali nchini chini ya chama cha madaktari wa ubongo na mshipa ya fahamu" amesema Dkt. Mbwanji.

Akiongea kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya Patrick Mwalunenge, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo Christopher Uhagile amesema Chama Cha Mapinduzi kimedhamiria kuwasaidia wananchi kupata huduma bora ikiwemo huduma za afya katika maeneo yao.

Uhagile amesema Mwenyekiti wa Chama hicho ametoa zaidi shilingi milioni 25 kwa ajili ya gharama zote za matibabu hayo ikiwemo kuwahudumia madaktari bingwa pamoja na mahitaji mengine.

Daktari bingwa wa mishipa ya fahamu Dkt. Boniface Kivevele amesema watajikita zaidi katika kutibu magonjwa ya mifumo ya fahamu pamoja na magonjwa ya watoto wachanga yanayoambatana na mgongowazi kwa kuwa magonjwa hayo hupelekewa matatizo ya mishipa ya fahamu.

Pia Dkt. Kivevele amesema huduma hiyo itatolewa pia kwa watu wazima wenye matatizo hayo pamoja na wale ambao matatizo yao yalitokana na ajali.

Nae daktari bingwa wa mifupa na majeraha Dkt. John Mbanga amesema wagonjwa wenye matatizo ya migongo watafanyiwa huduma ya upasuaji na huduma hiyo itaendelea hata mara baada ya kuondoka kwa madaktari bingwa.

No comments:

Post a Comment