Thursday, November 14, 2024

TDB KUHAMASISHA PROGRAMU YA UNYWAJI WA MAZIWA KUKABILIANA NA UDUMAVU

Serikali kwa kushirikiana na Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) imekuja na programu ya uhamasishaji unywaji maziwa ikilenga kuwafikia wanafunzi 100,000 katika shule 140 nchini.

Programu hiyo imefika katika mikoa nane ukiwepo Mkoa wa Mbeya sambamba na kutengeneza fursa ya usambazaji kwa wasindikaji wadogo kufikisha huduma mashuleni.

Kaimu Meneja wa Bodi ya Maziwa, Joseph Semu amesema jana Novemba 14, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na ujio wa programu hiyo kwa Mkoa wa Mbeya.

Ametaja lengo la serikali ni kuhamasisha wazazi kuona umuhimu wa kuwapatia wanafunzi maziwa watoto  badala ya vyakula vingine visivyo na protini mwilini

"Tunatambua maziwa yana virutubisho vingi mwilini hivyo mtoto akinywa anaweza kufanya vizuri kwenye masomo yake na kuchangia kuinua kiwango cha elimu kwa shule za msingi na kuondoa gharama" amesema.

"Programu imelenga kuzifikia Shule za Msingi 140 nchi nzima  zenye wanafunzi 100,000 kwa sasa wameifikia mikoa nane ukiwepo wa Mkoa Mbeya na Iringa" amesema

Ametaja mikoa mingine Kilimanjaro, Moshi, Morogoro, Kigoma, Dodoma, Tabora na Arusha huku  wakilenga kwa baadhi ya shule kwa kuangalia vigezo maalum kwa wahitaji.

Kwa upande wake Kaimu Ofisa Lishe Mkoa Lightness Shibone ameshukuru serikali kwa kuja na programu hiyo ambayo italeta chachu ya kupunguza tatizo la udumavu na utapia mlo kwa baadhi ya familia.

"Tutaendelea kuhamasisha wazazi kwa kutoa elimu kujua faida ya maziwa mwilini licha ya kuwepo kwa changamoto ya baadhi kuwa na uchumi duni na kutoweza kumudu kuhudumia familia" amesema.

Kwa upande wake Ofisa Mifugo Mkoa Dk. Samora Mshang'a amesema ili kufikia malengo wataendelea kutoa elimu kwa wafugaji kuzalisha maziwa kwa ubora utakaokidhi viwango.

Mshang'a amesema kwa Mkoa wa Mbeya kuna Halmashauri ya Rungwe na Busokelo zimekuwa zikifanya vizuri katika uzalishaji wa maziwa huku kwa siku wastani wa lita 240,000 upatikana

Licha ya kuwepo kwa programu hiyo baadhi ya wanafunzi wa Shule ya msingi Mwenge mchanganyiko wameomba serikali kuelekeza bajeti kwenye shule zenye uhitaji ili kuwezesha watoto kunywa maziwa na kuwa na uelewa wa masomo na kufanya vizuri.

No comments:

Post a Comment