Kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 nchini, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendesha mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari mkoani humo kuhusu masuala ya uchaguzi.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo Novemba 23, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Benki kuu ya Tanzania Tawi la Mbeya, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga amesema kuwa Jeshi la Polisi lipo imara kuhakikisha linasimamia sheria, kanuni na taratibu wakati wa uchaguzi na halitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayebainika kukiuka.
Kamanda Kuzaga amewataka Waandishi wa Habari kuwa wazalendo na kutumia taaluma yao kuwajulisha wananchi mchakato mzima wa uchaguzi jinsi unavyoenda na kutoa elimu kuhusu haki na wajibu wa mpiga kura.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoani Mbeya (Mbeya Press Club) ndugu Nebart Msokwa amelipongeza Jeshi la Polisi mkoani humo kwa jitihada mbalimbali za kuzuia na kutokomeza uhalifu hali inayopelekea wananchi kuishi na kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu.
Vile vile, Msokwa amelipongeza Jeshi la Polisi kwa ushirikiano linaloutoa kwa waandishi wa habari na kusisitiza kuendelea kushirikiana, kufanya vikao na mafunzo ya mara kwa mara ili kukumbushana masuala ya kiutendaji ikiwemo sheria na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.
Kwa upande wake Mkuu wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Charles Kinyongo ameeleza kuwa, Jeshi hilo limejipanga vizuri kuimarisha ulinzi na usalama kabla, wakati na baada ya uchaguzi na kuwaomba wananchi kutokuwa na hofu yoyote na kwenda kwenye vituo vya kupigia kura siku ya tarehe 27, 2024 ili kutimiza haki yao ya kidemokrasia ya kupiga kura kuwachagua viongozi ngazi ya Mitaa, Vitongoji na Vijiji.
No comments:
Post a Comment