Thursday, May 30, 2024

WANAOPANDISHA BEI YA VOCHA KUSHUGHULIKIWA

Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema wametoa maelekezo kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufuatilia wafanyabiashara wanaouza vocha za kukwangua kinyume na bei elekezi.

Maeneo mbalimbali nchini baadhi ya wafanyabiashara wamekua wakiuza Vocha ya Tsh 500/- kwa Tsh 600/- na vocha ya Tsh 1,000/- inauzwa kwa Tsh 1,200/-.

DC MALISA AAGIZA VIONGOZI ISYESYE KUFANYA MKUTANO WA WANANCHI

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa ameagiza viongozi wa Kata ya Isyesye Jijini hapa kuitisha mkutano wa wananchi kujadili changamoto mbalimbali na kuzitatua.

Malisa amesema jana Mei 29, 2024 kwenye mkutano wake wa kusikiliza kero za wananchi katika kata ya Isyesye jijini hapa ikiwa ni mkakati wake wa kupita kata kwa kata mtaa kwa mtaa sambamba na kuanzisha kliniki ya ardhi.

Miongoni mwa kero alizosikiliza ni pamoja ukosefu wa huduma ya maji,wizi wa mita za maji migogoro ya ardhi katika eneo la shule urasimishaji wa maeneo na fidia.

TIMU 32 KUWANIA MILIONI 11.4 ZA TULIA TRUST UYOLE CUP 2024

Mashindano ya mpira wa miguu maarufu kama Tulia Trust Uyole Cup 2024 yameanza kutimua vumbi jana Jumatano Mei 29, 2024  katika uwanja wa Mwawinji bonde la  uyole ya kati Jijini hapa.

Mashindano haya yanashirikisha timu 32 kutoka Jiji la Mbeya huku zawadi mbalimbali zikitolewa kwa washindi, sambamba na ugawaji wa vifaa vya michezo ikiwepo jezi, mipira kwa washiriki wa mashindano hayo.

Miongoni mwa zawadi zitakazotolewa kwa mshindi wa kwanza kitita cha Shilingi milioni tano, mshindi wa pili milioni, mshindi wa tatu atapata milioni mbili huku mshindi wa nne akiondoka na shilingi milioni moja.

Zawadi nyingine ni pamaoja na mfungaji bora Tsh 100,000/- kipa bora Tsh 100,000/- timu yenye nidhamu Tsh 100,000/- sambamba na kikundi bora cha ushangiliaji Tsh100,000/-.

Mashindano hayo yameandaliwa na Taasisi ya Tulia Trust ambayo Mkurugenzi wake ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya mjini Dkt. Tulia Ackson.

SUGU AMGALAGAZA MSIGWA UENYEKITI CHADEMA KANDA YA NYASA


Mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu), ameshinda nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa katika uchaguzi uliofanyika jana Mei 29, 2024 katika Mji mdogo wa Makambako.

Mbilinyi alishinda uchaguzi huo kwa kura 54 sawa na 51% akimshinda Mchungaji Peter Msigwa aliyekuwa akitetea nafasi hiyo aliepata kura 52 sawa na 49%. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti alishinda Frank Mwakajoka, Mbunge wa zamani wa Tunduma.

Wednesday, May 29, 2024

MBUNGE WA LUPA ARIDHISHWA UJENZI BARABARA YENYE UREFU KM 1.04

 

Mbunge wa Jimbo la Lupa Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya Masache Kasaka amefanya ziara ya  kukagua ujenzi wa miundombinu ya barabara yenye urefu wa kilometa 1.04.

Masache katika ziara yake ameambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwepo katibu wa CCM Wilaya Msafiri Mayeye na kwamba barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha rami.


Amesema ameridhishwa na utelezaji wa mradi huo ambao umelenga kutekekeza ilani ya uchaguzi ya 2020/2025 yenye kuleta maendeleo kwa wananchi.

Amesema mpaka ukamilike utagharimu zaidi ya Sh 397 milioni  ambayo na Serikali na kukamilika kwa mradi huo utakuwa kiungo kikubwa cha kuchochea shughuli za kiuchumi na mapato ya Serikali.

DC MALISA AHAMASISHA WANANCHI KUJIANDIKISHA DAFTARI LA MPIGA KURA

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa amewataka wananchi mkoani hapa  kujitokeza kwa wingi kujiandisha kwenye  maboresho ya dafrari la kudumu la wapiga kura  msimu utakapofika.

Malisa amesema jana Mei 28, 2024 kwa nyakati tofauti alipofanya  ziara ya kusikiliza kero  za wananchi katika kata za Tembela, Mwasanga na Kalobe Jijini hapa.

Amesema tunaelekea kipindi cha uchaguzi Mkuu Oktoba 2025 na uchaguzi mdogo wa Serikali za mitaa wananchi wanapaswa kuhamasika kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika  maboresho ya daftari la wapiga kura.


"Nitumie fursa hii kuwataka wananchi mjitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye maboresho ya dafrari la mpiga kura ili kupata fursa ya kuchagua  viongozi wazuri hata nyinyi mkitaka kugombea ni uhuru wa kidemokrasia kushiriki" amesema.

Friday, May 24, 2024

MASACHE AOMBA SERIKALI KUBORESHA VIWANJA VYA MICHEZO MBEYA

Mbunge wa Jimbo la Lupa Masache Kasaka ameiomba Serikali kuboresha uwanja wa Sokoine uliopo Jijini Mbeya na pia kukamilishwa kwa ujenzi wa uwanja unapatikana katika kata ya Mbugani wilayani Chunya.

Masache ameyasema hayo Bunge Jijini Dodoma wakati akichangia hotuba ya makadirio ya bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo iliyowasilishwa na Waziri mwenye dhamana Dkt. Damas Ndumbaro.

 "Mimi natoka Chunya, sisi tumepata bahati ya kupandisha timu ya ligi kuu msimu ujao KenGold FC, Mbeya sasa tuna timu mbili za ligi kuu Tanzania Prisons na KenGold FC, na timu moja ya daraja la kwanza Mbeya City, tunaiomba Serikali iboreshe uwanja wa Sokoine ili uwe bora zaidi, lakini pia sisi Chunya tulianza ujenzi wa uwanja wetu wa michezo, tunaiomba Serikali itupe fedha tukamilishe ule uwanja ili wanachunya waone sasa umuhimu wa kuwa na timu ya ligi kuu" amesema Masache.

Mbali na hayo Masache ameongeza kuwa fursa mbalimbali zitaendelea kufunguka wilayani Chunya endapo uwanja ukikamilika kwa wakati na timu ya KenGold FC kuutumia katika michezo yao ya nyumbani.

Friday, May 17, 2024

WALIOVAMIA HIFADHI MLIMA KAWETELE KUPEWA MAENEO

 Wakuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Kanali Denis Mwila wamekutana kutatua mgogoro wa wananchi na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) ambao wamevamia kwa ujenzi wa makazi na kilimo.

Uamuzi huo ni kutokana na maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera kwa wakuu hao wa Wilaya kukutana na TFS ili busara itumike kwa kuwaondoa katika hifadhi na kuwatengea eneo lenye ukubwa wa hekari 698.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 17, 2024 ikiwa ni siku moja imepita baada ya kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wa vijiji vya Ruiwa Wilaya ya Mbarali na Malamba Wilaya ya Mbeya.


Malisa amesema kutokana na uamuzi wa busara za Rais Samia Suluhu Hassan kupitia mkuu wa Mkoa wa Mbeya kuona thamani ya wakazi kwa kugawa maeneo yaliyohainishwa kwa ajili ya kilimo

Thursday, May 16, 2024

"WAANDISHI WA HABARI TUMIENI WELEDI KWENYE KAZI ZENU" DC MALISA


Serikali mkoani Mbeya imesema iko tayari kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari ili kuandika habari zenye kugusa jamii ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu na pia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Mbeya Beno Malisa wakati akimuwakilisha Mkuu mkoa wa Mbeya Juma Homera kwenye maadhimisho ya Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani ambapo kwa ngazi ya mkoa yamefanyika Mei 15, 2024 katika ukumbi wa Coffee Gadern jijini Mbeya.


Malisa amewataka waandishi wa habari mkoani hapa kutumia weledi na taaluma yao vizuri katika shughuli zao za kila siku. Pia amewataka waandishi kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazojitokeza kwenye maeneo yao.

Thursday, May 9, 2024

WACHIMBAJI MADINI YA DHAHABU CHUNYA WABURUZANA MAHAKAMANI


Mashauri matatu yaliyofunguliwa Mahakama ya Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya kwa hati ya dharula na Aidan Msigwa dhidi ya Lucas Mbwiga Mwapenza huhusiana na mgogoro wa kitalu cha uchimbaji madini ya dhahabu eneo la Kisumaini Kijiji cha Ifumbo Kata ya lfumbo Wilaya ya Chunya yamepokelewa na Hakimu James Mhanusi kwa ajili ya kusikilizwa.

Hati hiyo imewasilishwa Mahakama ya Wilaya ya Chunya na wakili wa kujitegemea Jacqueline Massawe kwa niaba ya Aidan Msigwa wakati Lucas Mbwiga Mwapenza akitetewa na Wakili Boniface Mwabukusi akisaidiwa na wakili Irene Mwakyusa.

Mashauri yaliyowasilishwa Mahakamani na wakili Jacqueline Massawe kwa niaba ya Aidan Msigwa ni pamoja na kesi ya msingi ya kutaka kumiliki eneo lake analodai kulimiliki kihalali baada ya kulinunua, shauri la pili ni kusudio la zuio la kutofanyika kwa shughuli zozote katika eneo hilo na shauri la tatu ni kuendelea na shughuli licha ya kuwepo Kwa zuio la Mahakama.