Wednesday, November 3, 2021

KESI YA MBOWE YAAHIRISHWA, SHAHIDI APATWA NA TATIZO LA KIAFYA

 

Shahidi wa sita katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe alitarajiwa kuanza kutoa ushahidi leo Jumatano Novemba 3, 2021 katika Mahakama Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Wakili wa Serikali Mwandamizi Robert Kidando, ameiomba Mahakama iahirishe kesi mpaka kesho kwa kuwa shahidi wao amepata tatizo la kiafya.

“Shauri linakuja kwa ajili ya kusikilizwa. mpaka jana kuna shahidi ambaye tulikuwa tumepanga kuendelea naye lakini amepata tatizo la kiafya. Hivyo tunaomba ahirisho mpaka kesho tutakapoweza kuendelea. Suala hili liko nje ya uwezo wetu,” amesema Kidando.

Kwa Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Peter Kibatala wamekubaliana na ombi hilo, lakini wakitaka upande wa mashtaka kuhakikisha wanaleta shahidi.

“Kwa kufuata amri ya Mahakama ya jana sisi tulikuwa tumejiandaa lakini kwa kuwa mambo yako hivi hatuna namna ila tunaomba tu wenzetu wajitahidi kesho tarehe 4 tuweze kuendelea,” amesema Kibatala.

Jaji Joachim Tiganga ameahirisha kesi hiyo hadi Kesho Alhamisi Novemba 4, 2021.

“Kufuatia maombi ambayo yameletwa na wakili Serikali kwamba shahidi waliyekuwa wamemwandaa amefika mahali hawezi kuja kutoa ushahidi kwa sababu zilizoelezwa za kiafya na kwa kuzingatia kuwa upande wa utetezi haukupinga basi maombi haya yanakubaliwa na shauri hili linaahirishwa hadi kesho.

“Upande wa mashtaka mnakumbushwa kuanda mashahidi ili tuweze kuendelea. Washtakiwa mtaendelea kuwa chini ya uangalizi wa Magereza,” ameeleza Jaji Tiganga.

Mbowe anakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi na kupanga kutekeleza ugaidi. Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Halfan Bwire Hassan (mshtakiwa wa kwanza), Adamu Hassan Kasekwa maarufu Adamoo na Mohamed Abdillahi Ling’wenya.

Monday, November 1, 2021

MAADHIMISHO YA WIKI YA MSAADA WA SHERIA 2021 KUFANYIKA KITAIFA MKOANI MBEYA

Mh. Juma Homera, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.

 Na Keneth Mwakandyali.

Wananchi mkoani wa Mbeya wametakiwa kujitokeza kwa wingi kutumia fursa ya Maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa Sheria inayofanyika kitaifa mkoani hapa kuanzia Novemba 01 hadi Novemba 12 katika viwanja vya Ruanda Nzovwe.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera leo Novemba alipokua akitoa akizungumza na waandishi wa Habari ambapo amewataka wananchi kuchangamkia fursa hii ili kuweza kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

“Kutakuwa na timu ya wataalamu watakaokua wanazunguka maeneo mbalimbali ya wazi, vizuizini, mashuleni kutoa elimu wa msaada wa kisheria katika Nyanja tofauti kama ardhi, ndoa, mirathi, haki za wanawake, watoto na watu wenye ulemavu kuanzia Novemba 01 mpaka Novemba 07”
 
“Kuna changamoto nyingi kwenye secta hii ndio maana shughuli hii ya wiki wa msaada wa kisheria kufanyika kitaifa mkoani Mbeya inakwenda kuleta fursa kwa wananchi wenye changamoto mbalimbali kuweza kujua haki zao” alisema Homera
 
Naye mratibu wa Chama cha Sheria Tanganyika Kanda ya Mbeya Gerinus Mzanila amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupata fursa ya kuweza kusaidiwa changamoto za kisheria walizonazo na kujitanua katika nyanja za kisheria.
 
“huduma ya msaada wa kisheria ni huduma ambayo inatolewa kwa mtu ambae hana uwezo wa kumudu gharama za huduma ya kisheria, zile ambazo zinatolewa mahakamani au kwa wakili. Huduma ya kisheria ipo katika nyanja nyingi kama vile kumuhoji na kusikiliza jambo lake, kumsaidia kuandaa nyaraka anazotakiwa kwenda kuzisajili mahakamani, usuluhishi wa amani, pia kutoa elimu kuhusiana na mambo mbalimbali ya kisheria” amesema Mzanila 
 
Aidha Afisa Maendeleo ya Jamii  Mkoa wa Mbeya Stella Kategile ameeleza kuwa wiki ya msaada wa kisheria imekua msaada mkubwa katika jamii kwani imejikita zaidi katika kutoa msaada kwa wananchi ambao hawana kipato na kushindwa kumudu gharama za huduma ya kisheria.

Saturday, August 21, 2021

TANLAP YAWANOA WANAHABARI MBEYA


 Na Hannelore Mrosso,

Mtandao wa watoa msaada wa sheria Tanzania (TANLAP) umeendesha mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari mkoani Mbeya ili kuwaongezea uelewa juu ya umuhimu wa kuzingatia sheria inayosimamia utoaji wa huduma ya habari katika utendaji kazi wao wa kila siku.

Mafunzo hayo yamefanyika Agosti 20 mwaka huu yakihusisha watendaji mbalimbali kutoka taasisi isiyo ya kiserikali inayotoa msaada wa kisheria ijulikanayo kama SAUTI YA HAKI.

Kaimu mkurugenzi mtendaji wa TANLAP Bw. Machereli Machumbana amewaambia waandishi wa habari kuwa mtandao huo ulianzishwa mwaka 2006 na kusajiliwa mwaka 2009 ambapo mpaka sasa una wanachama 76, unalenga kuwakumbusha wanahabari kuhusu sheria mbalimbali zinazoongoza na kusimamia tasnia ya habari ili kuepuka kukinzana na sheria hizo hatimaye kujikuta wanakumbana na makosa ya kisheria.

Saturday, May 22, 2021

WAHITIMU KIDATO CHA SITA 2021 WAITWA NA JKT


Wahitimu wa kidato cha sita mwaka 2021 wametakiwa kuhudhuria mafunzo kwa mujibu wa sheria katika kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) walizopangiwa  kuanzia Juni Mosi hadi 10, 2021.

Hayo yamesemwa jana Jumamosi Mei 22,  2021 na Kaimu mkuu wa utawala wa JKT, Kanali Hassan Mabena huku akizitaja kambi hizo kuwa ni Rwamkoma Mara, Msange Tabora, Ruvu Pwani, Mpwapwa, Makutupora Dodoma, Mafinga Iringa, Mlale, Itaka Songwe, Luwa, Milundikwa Rukwa, Nachingwea Lindi na Kibiti Pwani.

Kambi nyingine ni Oljoro JKT Arusha, Mgambo, Maramba Tanga, Makuyuni Arusha, Bulombora  na Mtabila Kigoma.

TULIA TRUST YASAIDIA UJENZI WA MATUNDU YA VYOO SHULE YA MSINGI ILOMBA

Na Ezekiel Kamanga.

Taasisi ya Tulia Trust inayoongozwa na Naibu Spika na Mbunge wa Mbeya Mjini Dkt Tulia Ackson imeungana na wananchi wa Kata ya Isyesye Jijini Mbeya katika ujenzi wa matundu nane ya vyoo shule ya msingi Ilomba inayokabiliwa na upungufu wa matundu ishirini na nane.

Zoezi hilo liliongozwa na Meneja wa Tulia Trust Jacqueline Boaz ambaye lengo ni kuunga mkono juhudi za wanachi wa Isyesye kwa kuchimba mtaro na kusomba mawe ili vyoo vikamilike kwa wakati ili kupunguza changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo katika shule hiyo.

"Hii si mara ya kwanza kutembelea shule hii mwaka 2019 Dkt Tulia alifika hapa kutoa msaada wa mifuko mia ya saruji na tanki la maji baada ya kupokea mahitaji kutoka kamati ya shule kwa ajili ya ukarabati wa madarasa", alisema Jacqueline.

Sunday, May 9, 2021

DKT. TULIA, MARYPRISCA, FYANDOMO WATOA MSAADA KWA WAHANGA WA MAFURIKO WILAYANI KYELA NA BUSOKELO

Pichani ni Naibu Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson (katikati), Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (kulia), na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya Mh. Suma Fyandomo (kushoto).

 
HABARI NA EZEKIEL KAMANGA.

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Ackson, Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi ambaye ni Mbunge wa Wanawake Mkoa wa Mbeya na Suma Ikenda Fyandomo Mbunge wa Wanawake Mkoa wa Mbeya wamewatembelea kuwapa faraja na kutoa msaada wa chakula kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko Wilaya ya Kyela na Busokelo Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.

Akitoa taarifa Kijiji cha Kisale Kata ya Ipinda kwa viongozi hao Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela Ezekiel Magehema alisema baadhi ya wananchi chakula kimeharibika, nyumba zao zimeboka pia mazao yamesombwa na maji hivyo wanawakati mgumu wa kujikimu ambapo baadhi wamehifadhiwa na ndugu zao.

Wednesday, May 5, 2021

MV MBEYA II KUSITISHA SAFARI ZAKE KWA MUDA


Huduma za safari za meli ya Mv Mbeya II zimesitisha kwa muda kwaajili ya kuifanyia uchunguzi baada ya kupigwa na mawimbi hadi kupelekea kukwama kwenye mchanga ikiwa safarini katika Ziwa Nyasa.

Akizungumza na chombo kimoja habari leo Jumatano Mei 5, 2021 Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Claudia Kitta amesema abiria waliokuwa katika meli hiyo walioshindwa kurejea majumbani mwao baada ya tukio hilo watarejeshewa nauli zao, watapewa chakula na maradhi.

"Meli ya Mv Mbeya II kwa sasa haitoweza kuendelea na safari mpaka itakapofanyiwa uchunguzi wa kina wa kitaalam na tukijiridhisha itaruhusiwa kuendelea na safari na baadhi ya abiria wamewezeshwa sehemu ya maradhi ya chakula mpaka watakapoanza safari ya kwenda walikokuwa wakienda,” amesema Kitta.

Amesema kikao cha kamati ya ulinzi na usalama kitafanyika kwa ajili ya kufanya tathmini ya mahitaji ya Wananchi waliokuwa safarini mpaka uchunguzi wa meli hiyo utakapokamilika na kuendelea na safari.

Aidha, amesema baadhi ya abiria walipanda mabasi baada ya kurejeshewa nauli.

Monday, May 3, 2021

UFAFANUZI WA SPIKA NDUGAI KUHUSU UBUNGE WA AKINA HALIMA MDEE NA WENZAKE

 

"Aandike barua aambatanishe na katiba ya chama chake, aniambatanishie na muhtasari wa hicho kikao kilichofanya hayo maamuzi, inawezekana huyo Katibu Mkuu kaamka tu kaandika halafu na mimi nakurupuka nachukua hatua, nitakua ni Spika au kitu cha ajabu, hivyo andika ili ile barua niwape watalam waangalie, halafu namuuliza msajili wa chama hawa wajumbe walioorodheshwa ndiyo wajumbe halisi?", amesema
 Spika Ndugai

UJUMBE WA BALOZI WA SWEDEN TANZANIA KWA UMOJA WA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA

Balozi wa Sweden Tanzania, Mh. Anders Sjöberg.

"Mimi kama Balozi wa Sweden ninafurahi kuwepo leo kusherekea uhuru wa habari na kujieleza. Sweden na Tanzania ni marafiki wa siku nyingi, na wote tunatambua kwamba nguzo hii, sambamba na haki ya kupata taarifa ni muhimu sana kwa jamii inayoheshimu Demokrasia na Haki za Binadamu".

"Sweden inaamini kwamba maendeleo ya nchi yoyote ile yanapatikana kwa kupeana tarifa, kujadiliana kwa uwazi, na kuwajibishana. Basi sisi tutaendelea kuungana na watanzania wote katika jitihada za kukuza na kuendeleza uhuru wa habari na kujieleza nchini". Balozi Anders Sjöberg



Wednesday, March 17, 2021

WATAALAMU WA DAWA ZA USINGIZI WAASWA KUENDELEZA UJUZI WA ELIMU WALIYOPATA

 Na Esther Macha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji  amewaasa watalaam wa utoaji salama wa  dawa za usingizi katika shule ya dawa za usingizi iliyopo Hospitali ya Rufaa ya Kanda hiyo kuwa wanaporudi kwenye vituo vyao vya kazi kuendeleza ujuzi, elimu waliyopata pamoja na ushirikiano walioupata ili kuboresha huduma za upasuaji nchini.

Aidha Mkurugenzi huyo amewataka watalaam hao kujikita katika mbinu nyingine ya kujiongezea kipato ili kustawisha uchumi wao binafsi.
 Dkt . Mbwanji alisema hayo jana wakati wa wa mahafali ya kwanza ya mafunzo ya utoaji dawa za usingizi kwa wahitimu 36 mafunzo ambayo yamefanyika kwa muda wa mwaka mmoja katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya

Monday, March 15, 2021

MAMA SAMIA: CHAPENI KAZI, MSIBABAISHWE NA MANENO YA WALIO NJE YA NCHI

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka watanzania kushikamana na kutobabaishwa na maneno yanayozungumzwa na watu walioko nje ya nchi akiwahikikishia nchi iko salama.

Alisema hayo leo alipokuwa akiweka jiwe la msingi ujenzi wa jengo la ghorofa moja la Halmashauri ya Wilaya ya Handeni vijijini linalojengwa mjini Mkata.

Samia alisema ni kawaida kwa binadamu kupata hitilafu katika mwili kama mafua na kuwataka  watanzania kushikamana na kuliombea Taifa.


"Hakuna wakati muhimu ambao watanzania wanatakiwa kushikamana na kuliombea Taifa kama wakati huu," alisema Suluhu.

"Niwahakikishie wananchi wenzangu Tanzania tupo salama, chapeni kazi ili kuleta maendeleo... msibabaishwe na maneno ya watu walioko nje ya nchi," alisema Samia ambaye ameanza ziara ya siku tano mkoani Tanga.

Alielekeza kufurahishwa kwake na mradi wa ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Handeni Vijijini ambalo linatarajiwa kugharimu sh 5.3 bilioni.

Wednesday, January 20, 2021

WAZIRI MKUU AAGIZA HALMASHAURI ZINAZOLIMA MKONGE KUANZISHA VITALU VYA UZALISHAJI WA MICHE YA MIKONGE

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo Jumatano, Januari 20, 2021 amekagua kitalu cha miche ya mkonge cha TARI Mlingano kilichopo wilayani Muheza, Tanga na kufungua zoezi la ugawaji wa miche kwa wakulima wa zao hilo.

Akizungumza wakati wa tukio hilo Waziri Mkuu ameziagiza Halmashauri zinazolima mkonge nchini pamoja na wakulima wakubwa wa mkonge watenge ekari 10 kwa ajili ya kuanzisha vitalu vya kuzalisha miche ya mkonge ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa miche ya mkonge
 
Amesema kituo cha TARI Mlingano kinatakiwa kijikite katika kufanya  utafiti wa mbegu bora pamoja na dawa za kudhibiti magonjwa katika zao hilo na suala la uzalishaji wa mbegu lifanywe kwa ushirikiano katika ya kituo hicho na wadau wa zao hilo.

Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo itenge fedha katika bajeti yake kwa ajili ya kituo cha TARI Mlingano ili kukiwezesha kupanua eneo la uzalishaji miche kwa kununua vitendea kazi yakiwemo matrekta.