Sunday, May 9, 2021

DKT. TULIA, MARYPRISCA, FYANDOMO WATOA MSAADA KWA WAHANGA WA MAFURIKO WILAYANI KYELA NA BUSOKELO

Pichani ni Naibu Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson (katikati), Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (kulia), na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya Mh. Suma Fyandomo (kushoto).

 
HABARI NA EZEKIEL KAMANGA.

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Ackson, Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi ambaye ni Mbunge wa Wanawake Mkoa wa Mbeya na Suma Ikenda Fyandomo Mbunge wa Wanawake Mkoa wa Mbeya wamewatembelea kuwapa faraja na kutoa msaada wa chakula kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko Wilaya ya Kyela na Busokelo Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.

Akitoa taarifa Kijiji cha Kisale Kata ya Ipinda kwa viongozi hao Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela Ezekiel Magehema alisema baadhi ya wananchi chakula kimeharibika, nyumba zao zimeboka pia mazao yamesombwa na maji hivyo wanawakati mgumu wa kujikimu ambapo baadhi wamehifadhiwa na ndugu zao.
 
Magehema alisema wanazo kamati za maafa kutoka ngazi ya Wilaya, Kata na Vijiji ambazo zinabaini wahitaji wa msaada wa hali na mali zinazohusika na ugawaji wa misaada inayotolewa.
 
Hata hivyo alisema pia baadhi ya maeneo miundo mbinu ya umeme, maji na barabara imeharibiwa hivyo kuwapa wananchi wakati mgumu pia kuleta kadhia ya usafiri kutokana barabara kukatika ambapo serikali inaendelea kufanya tathimini ili kuona msaada gani unahitajika hivyo aliwashukuru Naibu Spika, Naibu Waziri wa Maji na Mbunge kufika kwa haraka mbali ya kuwafariji lakini wametoa msaada wa chakula kwa wahanga.

 
Kabla ya kukabidhi msada wa chakula Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi alisema wameshtushwa na tukio hilo hivyo wamelazimika kuja kutoa faraja japo kwa kidogo ili kuungana na wahanga waliokumbwa ikiwa ni ishara ya upendo kwani maafa ni makubwa wamejionea baadhi ya wananchi kukosa makazi, chakula kusombwa na mazao kuzama na maji.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya Suma Fyandomo alisema maafa hayo kwa wananchi walipewa taarifa na Mbunge wa Kyela Ally Jumbe Mlagila hivyo wameungana naye katika kipindi hiki kigumu kinachowakabili wananchi wake hivyo aliwataka wananchi kumuomba Mungu ili kuwaepusha na majanga.

Aidha Fyandomo aliiomba wananchi kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuiongoza nchi kwa uweledi pia aangalie namna ya kuisaidia Wilaya ya Kyela ambayo ipo hatarini kukumbwa na njaa kutokana na mazao kusombwa na maji.

 
Akikabidhi chakula kilichotolewa kilo mia sita hamsini za unga, kilo mia mbili arobaini za maharagwe na kilo mia mbili za mchele Naibu Spika Dkt. Tulia alisema tukio hilo wamelipokea kwa masikitiko makubwa kupitia kwa Mbunge wa Kyela na alisema anafuatilia ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha maafa ili kuona namna ya kuwasaidia wananchi wa Kyela.

Dkt. Tulia alisema kaya nyingi zimeathiriwa na mafuriko ameshauri kipaumbele kiwe kwa wenye uhitaji mkubwa kwani wao wanafahamiana.

Alisema wamejionea hali halisi hivyo wataungana na Mbunge wa Kyela pindi atakapowasilisha hoja hiyo Bungeni katika vikao vinavyoendelea.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisale Jackson Mwakambulo alisema wanaishukuru serikali kwa hatua ya haraka waliyoichukua ili kukabiliana na janga hilo.

"Nichukue fursa hii kuiomba serikali kuomba msaada wa mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi ili tuweze kukabiliana na njaa" alisema Jackson.

Baadhi ya wananchi akiwemo Frola Lukuta na Hosea Mwankenja mbali ya kuishukuru serikali  pia viongozi waliofika kutoa msaada wa chakula.

Ziara hiyo iliendelea Kijiji cha Mpunguti Kata ya Luteba ambapo Diwani wa Kata hiyo Ayub Mwalubona alisema mtu mmoja amefariki na nyumba ishirini na nane zimeanguka na miundo mbinu ya barabara na umeme imeharibika.
 
Nae mwenyekiti wa Kijiji Sadiki Mwakalukwa ameshukuru viongozi hao kwa kuwajali na kuwapa faraja.

 

No comments:

Post a Comment