Wednesday, March 17, 2021

WATAALAMU WA DAWA ZA USINGIZI WAASWA KUENDELEZA UJUZI WA ELIMU WALIYOPATA

 Na Esther Macha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji  amewaasa watalaam wa utoaji salama wa  dawa za usingizi katika shule ya dawa za usingizi iliyopo Hospitali ya Rufaa ya Kanda hiyo kuwa wanaporudi kwenye vituo vyao vya kazi kuendeleza ujuzi, elimu waliyopata pamoja na ushirikiano walioupata ili kuboresha huduma za upasuaji nchini.

Aidha Mkurugenzi huyo amewataka watalaam hao kujikita katika mbinu nyingine ya kujiongezea kipato ili kustawisha uchumi wao binafsi.
 Dkt . Mbwanji alisema hayo jana wakati wa wa mahafali ya kwanza ya mafunzo ya utoaji dawa za usingizi kwa wahitimu 36 mafunzo ambayo yamefanyika kwa muda wa mwaka mmoja katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya MbeyaHata hivyo Mkurugenzi huyo alishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto kwa kutoa idhini ya kuanzishwa kwa shule hiyo ya mafunzo ya kutoa za dawa za usingizi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya mwaka 2019.

"Raha ya kufanya kazi katika chumba cha upasuaji ni kila mmoja kuona umuhimu wa mwenzake bila kujali ngazi ya elimu yake, hivyo nitoe wito mnaporudi huko mkafanye kazi kwa ushirikiano na kutambua umuhimu wenu na wa wengine." alisema Dkt Mbwanji

Akishukuru kwa niaba ya wahitimu wenzake Sir Sabina Mwilongo kutoka kituo cha afya St. Vincet Vikindu kilichopo Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani, alishukuru uongozi wa hospitali kwa kuona umuhimu wa kuanzishwa kwa mafunzo ya utoaji dawa za usingizi pamoja na juhudi za wakufunzi na ushirikiano wa wafanyakazi wa hospitali katika kufanikisha mafunzo hayo na kuahadi kwenda kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kwa kuzingatia ujuzi waliopewa.

Kwa upande wake Mkuu wa idara ya ganzi na dawa za usingizi Dkt. Amos Muzuka alisema kuwa wahitimu hao zaidi ya kupatiwa mafunzo ya  utoaji salama wa dawa za usingizi vilevile wamepatiwa ujuzi katika idara mbalimbali ikiwemo ya wagonjwa mahututi (ICU) na idara ya magonjwa ya dharura na ajali (Emergence Department).

No comments:

Post a Comment