Saturday, May 22, 2021

TULIA TRUST YASAIDIA UJENZI WA MATUNDU YA VYOO SHULE YA MSINGI ILOMBA

Na Ezekiel Kamanga.

Taasisi ya Tulia Trust inayoongozwa na Naibu Spika na Mbunge wa Mbeya Mjini Dkt Tulia Ackson imeungana na wananchi wa Kata ya Isyesye Jijini Mbeya katika ujenzi wa matundu nane ya vyoo shule ya msingi Ilomba inayokabiliwa na upungufu wa matundu ishirini na nane.

Zoezi hilo liliongozwa na Meneja wa Tulia Trust Jacqueline Boaz ambaye lengo ni kuunga mkono juhudi za wanachi wa Isyesye kwa kuchimba mtaro na kusomba mawe ili vyoo vikamilike kwa wakati ili kupunguza changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo katika shule hiyo.

"Hii si mara ya kwanza kutembelea shule hii mwaka 2019 Dkt Tulia alifika hapa kutoa msaada wa mifuko mia ya saruji na tanki la maji baada ya kupokea mahitaji kutoka kamati ya shule kwa ajili ya ukarabati wa madarasa", alisema Jacqueline.

Dour Issah Mohammed ni Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya aliungana na wananchi wa Isyesye na kuahidi Halmashauri itaungana na wananchi hao ili kukamilisha matundu hayo kwa wakati.

"Nampongeza Mbunge kwa kusaidia kukamilisha miundo mbinu ya afya na elimu katika Jiji la Mbeya kupitia Taasisi ya Tulia Trust" alisema mstahiki Meya.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Isyesye Ibrahimu Mwampwani alisema ujenzi wa matundu ya vyoo ni utekelezaji wa mkutano wa wazazi ulioazimia kuanza haraka ujenzi wa matundu ya vyoo ili kuwaondolea adha wanafunzi.

"Shule inakabiliwa na upungufu wa matundu ishirini na nane na mpaka sasa tumefanikiwa kukusanya shilingi laki saba na elfu ishirini na mabati mawili kwa ajili ya ujenzi", alisema Mwampwani.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule ya Ilomba Edward Joel alisema kukamilika kwa matundu hayo kutapunguza msongamano katika maliwato ambapo baadhi ya matundu ya vyoo kwa sasa hayatumiki kutokana na uchakavu.

Daniel Mbalamwezi, Samson Manda, Vumilia Ambonisye, Mwafrika Sanga na Mary Mbuza ni baadhi ya wananchi waluojitokeza katika ujenzi kwa nyakati tofauti mbali ya kuipongeza Taasisi ya Tulia Tulia Trust kujitokeza kuwaunga mkono katika ujenzi wamewaomba wazazi kujitokeza kukamilisha matundu hayo kwa wakati.

"Mimi ni mzazi nimejitokeza kuitikia wito wa viongozi waliotutaka kujenga matundu ya vyoo ili kuwaondolea usumbufu watoto wetu" alisema Vumilia Ambonisye.

Kukamilika kwa matundu nane kutapunguza kwa kiasi msongamano wa wanafunzi katika maliwato hivyo kusalia matundu ishirini ili kumaliza kabisa tatizo la uhaba wa matundu ya vyoo.



No comments:

Post a Comment