Saturday, August 21, 2021

TANLAP YAWANOA WANAHABARI MBEYA


 Na Hannelore Mrosso,

Mtandao wa watoa msaada wa sheria Tanzania (TANLAP) umeendesha mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari mkoani Mbeya ili kuwaongezea uelewa juu ya umuhimu wa kuzingatia sheria inayosimamia utoaji wa huduma ya habari katika utendaji kazi wao wa kila siku.

Mafunzo hayo yamefanyika Agosti 20 mwaka huu yakihusisha watendaji mbalimbali kutoka taasisi isiyo ya kiserikali inayotoa msaada wa kisheria ijulikanayo kama SAUTI YA HAKI.

Kaimu mkurugenzi mtendaji wa TANLAP Bw. Machereli Machumbana amewaambia waandishi wa habari kuwa mtandao huo ulianzishwa mwaka 2006 na kusajiliwa mwaka 2009 ambapo mpaka sasa una wanachama 76, unalenga kuwakumbusha wanahabari kuhusu sheria mbalimbali zinazoongoza na kusimamia tasnia ya habari ili kuepuka kukinzana na sheria hizo hatimaye kujikuta wanakumbana na makosa ya kisheria.

"Sisi kama TANLAP tunaendelea kufanya kazi na waandishi wa habari ili kuhakikisha kwamba tunakuwa na jamii inayozingatia uhuru wa kutoa mawazo, uhuru wa kujumuika na kuheshimu uhuru wa kidemokrasia katika nchi huru kama Tanzania" ameeleza Machumbana.

Kwa upande wake mwezeshaji wa mafunzo hayo wakili James Marenga ambaye pia ni mwanahabari mwandamizi, amewataka waandishi wa habari waache kuandika habari zinazochochea ugaidi badala yake wajikite katika kuibua masuala yanayolenga kuboresha mahusiano ya umma.

"Tasnia ya habari ni ghali sana duniani hivyo ni wajibu wenu kuitunza kwa gharama yoyote, hakikisheni hamchochei vurugu kwenye jamii kwa kuzingatia sheria ya huduma za habari ya mwaka 2016 na ile ya makosa ya mtandaoni ya mwaka 2015 kila wakati mnapotekeleza majukumu yenu" ameeleza wakili huyo.

Aidha wakili Marenga amesisitiza kwamba wanahabari nchini wanapaswa kujiendeleza kielimu ili kutimiza takwa la kisheria.

"Kuhusu kujiendeleza kitaaluma ili kupata astashahada ya habari hilo halina mjadala nendeni shule ili kuiongezea thamani tasnia hii" amefafanua zaidi wakili huyo.

Nao waandishi wa habari waliopata fursa ya kushiriki mafunzo hayo wameupongeza na kuushukuru mtandao wa TANLAP kwa kuandaa mafunzo hayo kwani yatawasaidia kutekeleza majukumu hayo kwa weledi zaidi na kuepuka makosa ya kisheria.

No comments:

Post a Comment