Wednesday, January 10, 2024

WANAUME KUTOSHIRIKI KLINIKI KUNACHANGIA KUTOTENGWA BAJETI ZA LISHE KATIKA FAMILIA

Wadau wakiwemo wazazi wakiwa katika kituo maalumu cha Malezi Jumuishi kilichofunguliwa na Taasisi ya WeCare Foundation kwaajili ya kutoa elimu ya afua za malezi stahiki kwa watoto ikiwemo lishe bora katika Hospitali ya Agakhan tawi la Mbeya. (Picha na Joachim Nyambo)

 

Hatua ya wanaume kutohudhuria kliniki wakati wenza wao wakiwa wajawazito au wanapokuwa wamejifungua inatajwa kuwa chanzo cha familia nyingi kutotenga bajeti ya milo sahihi kwa wanawake wajawazito, wanaonyonyesha na pia watoto wanaotimiza umri wa miezi sita tangu kuzaliwa.

 

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa Makala haya umebaini kuwa licha ya wadau mbalimbali zikiwemo Taasisi binafsi na za serikali kutilia mkazo suala la uhamasishaji wanaume kuhudhuria kliniki pamoja na wenza wao bado mwamko ni mdogo.

 

Wadau wakiwemo wauguzi waliozungumzia hali hiyo wanasema ni wanaume wachache ambao wanaona umuhimu wa kwenda na wenza wao kliniki wanapokuwa wajawazito au wanapowapeleka watoto wachanga.

 

Muuguzi Priscar Mwalwega kutoka Hospitali ya Agakhan tawi la Mbeya alisema hata wanaume wanaowasindikiza wenza wao hospitalini hapo hupenda kuondoka na kuwaacha hata kabla ya kupewa huduma wakifikiri hakuna umuhimu wa wao kubaki wapewe maelekezo kwa pamoja.

 

“Wachache wanawasindikiza wenza wao hasa wale walio na vyombo vya usafiri. Lakini wanapofika utasikia wanauliza si naweza kuondoka tu nikamuacha maana nawahi kwenye majukumu. Hapo inabidi tunawaelewesha kuwa ni muhimu na wao wakasikiliza maelekezo yanayotolewa ili wakirudi nyumbani wawakumbushe mambo muhimu wenza wao ikiwemo milo sahihi kwa wajawazito, mama anayenyonyesha au chakula kwa mtoto aliyetimiza miezi sita". Alisema Mwalwega

 

“Lakini kwakuwa tunasema baba ni kichwa cha nyumba tunaamini kuwa hata kwenye suala la kutenga bajeti anaweza akawa na sauti zaidi hivyo akiwa na uelewa wa kutosha juu ya lishe sahihi kwa wajawazito, wanaonyonyesha au watoto wadogo itakuwa rahisi eneo hilo kupewa kipaumbele wanapopanga".  Aliongeza.

 

Mwalwega alisema kupitia kituo cha elimu ya Malezi na Makuzi ya Awali ya Mtoto walichofungua walichofungua kwa kushirikiana na Taasisi ya WeCare Foundation wanaendelea kutoa elimu kwa wanaume wanaofika na wake zao juu ya umuhimu wa kushiriki masuala ya kliniki juhudi alizosema zinaonekana kuleta matukio chanya kwa baadhi kuhamasika.

 

“Wanaofika pale kituoni tukiwapa elimu wanaonyesha kuhamasika..nadhani walio wengi hawashiriki kutokana na kukosa uelewa kwakuwa tumeshuhudia wale wanaokuja wakiondoka wanakuwa na mabadailiko na wanaendelea kuja japo mara moja moja".

 

Afisa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Itika Mlagila alisema kutokana na wanaume kukosa elimu ya lishe bora kwa wajawazito, wanaonyonyesha na pia watoto wachanga familia hazitengi bajeti za baadhi ya makundi ya vyakula ambavyo ni muhimu kwenye ukuaji wa watoto.

 

Mlagila alitolea mfano kwa kundi ambalo halipewi kipaumbele na familia nyingi kuwa ni la Protini yaani la vyakula vya mazao ya jamii ya wanyama pamoja na wadudu wote wanaoliwa kulingana na taratibu na imani za watu mbalimbali kama maziwa, nyama, mayai, kumbikumbi na senene.

 

“Kundi hili linaitwa Protini au Utomwili na kazi yake kubwa ni kuujenga mwili. Hivyo kundi hili ni kama matofali yanayowezesha kuujenga mwili yaani itasababisha mtoto akue kiurefu, aongezeke ukubwa wa ubongo wake na aweze kuzalisha tishu mbalimbali zenye muonekano wa afya bora kama ngozi, kucha na nyinginezo".

 

“Na kundi hili asilimia kubwa ya watoto wetu hawapatiwi na wazazi wengi hawaamini kama mtoto akishafikisha umri wa miezi sita kama anaweza akala nyama au akala samaki, wanaamini anaweza kula uji tu. Na takwimu zinaonesha hata hapa kwetu Mbeya wazazi wengi hawalipi umuhimu kundi hili". Aliongeza.

 

Anasema katika kuhimiza lishe bora kwa wajawazito, wanaonyonyesha na watoto wadogo Halmashauri imeweka utaratibu wa wataalamu wa lishe kupita katika mitaa na kutoa elimu lishe kwa kila mtaa kila baada ya miezi mitatu.

 

Anasema kupitia programu hiyo wamefanikiwa kuwafikia watu wengi na tayari mafanikio yameanza kuonekana ikiwemo ufuatiliaji wa maendeleo ya afya ya watoto wanaokutwa na changamoto zinazotokana na lishe duni.

 

“Tukiwa katika mtaa tunaitumia siku hiyo kufundisha naana ya kuandaa vyakula vya aina mbalimbali muhimu kwa lishe lakini pia tunawapima watoto na wale wanaoonekana wana changamoto tunaanza kuwafuatilia mpaka pale wanapoimarika na hapo wazazi wao na wao wanakuwa wamepata uelewa wa kutosha na kuzingatia makundi ya vyakula".

 

Mafanikio mengine ni kuwafikia wanaume kwa urahisi kwakuwa wanawakuta kwenye maeneo wanayoishi hivyo kwa wale wanaokuwa na nafasi wanahudhuria na kupata elimu pamoja na wenza wao na jamii ya mitaa husika kwa ujumla.

 

“Tunaitumia siku hiyo kutoa elimu si kwa wazazi walio na watoto au wajawazito pekee ni kwa jamii yote na ndiyo maana tunaiita siku ya afya ya lishe ya mtaa. Japo kwa wajawazito na walio na watoto walio na umri wa chini ya miaka mitamo ni lazima na wasiofika wanatozwa faini Shilingi elfu kumi".

 

Jenipha Antony ni Afisa miradi kutoka Shirika la Shalom lililo na jukumu la kuchechemua utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Makuzi, Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) mkoani Mbeya ambaye anasema utoaji elimu ya lishe bora na uhamasishaji wanaume juu ya masuala ya kliniki kwa wajawazito na wanaonyonyesha inapaswa ifanyike pia kwenye mikusanyiko mingine ya kijamii ikiwemo katika masoko.

 

Alisema kwakuwa wanaume wengi wanatoa visingizio vya shughuli za kiuchumi ni vema kwa wale ambao shughuli zao zinakuwa za mikusanyiko kama wafanyabiashara wafuatwe wanakofanyia ili na wao waweze kupata elimu stahiki.

 

“Kama tunaweza kuwafuata mitaani kwao tuone pia sababu ya kuwafuata kule wanakofanyia shughuli za kujiingizia kipato. Kwenye masoko kama Mwanjelwa, Sido au Soweto wengi wanashinda huko na huenda mtaani hatuwakuti na kliniki hawaji sasa tukiwafuata itawarahisishia kupata elimu.”

No comments:

Post a Comment