Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira akitoa maelekezo kwa watendaji wa mmoja wa migodi alitotembelea Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya.
Serikali imepiga marufuku shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu na kuchenjua katika Mto Zira Kata ya Ifumbo Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya mpaka wataalam watakapofika kufanya tathimini ya mazingira.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Seleman Jaffo, amesema hayo juzi wilayani Chunya wakati akiwa kwenye ziara ya kutembelea Kampuni ya G&I ambayo ilisitishiwa uzalishaji katika mto huo.
Jaffo amesema katika ziara yake miongoni mwa maeneo yaliyo msukuma ni kujiridhisha shughuli za uchimbaji zinazofanywa kwenye mto huo, sambamba na kutoa mwelekeo wa Wizara kutoruhusu shughuli hizo mpaka wataalam watakapofanya tathimini.
“Nimefika hapa kujiridhisha kwani awali nilituma wataalam kutoka Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanya tathimini ya hali ya Mazingira na kutoa maelekezo ambayo yalipuuzwa” amesema Jaffo.
Jaffo amesema suala lingine ni idadi kubwa ya maombi ya vibali 100 vya kufanya tathimini ya Mazingira vilivyofikishwa ofisini kwake hali iliyomshtua na kuona kuna umuhimu wa kufika eneo hilo ambalo lina utajiri mkubwa wa dhahabu.
“Nimefika nimeona hali halisi ni kweli Serikali tunawapenda wawekezaji msimamo wangu eneo hilo isitoke dhahabu wala kuchenjua ndani ya mto mpaka hapo wataalam watakapofanya tathimini ya mazingira kwa kuwashirikisha wananchi na wawekezaji ndani ya mto huo” amesema Jaffo.
Amesema atopenda kusikia uzalishaji ukiendelea na kuagiza NEMC Kanda ya Nyanda za Juu na Makao Makuu kuingia kazini kwa kuishirikisha jamii na wawekezaji hao.
Wakati huo huo ameagiza wamiliki wote wa migodi ya dhahabu Wilaya ya Chunya kuwa na mabwawa ya kutililisha maji ya tope lenye sumu ili kulinda afya za Wananchi
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema uamuzi huo wa Waziri ni sahihi na kuna sababu ya wawekezaji kugeukia teknolojia za kisasa ili kuepuka madhara ya kemikali kwenye maji.
Mkurugenzi uzingatiaji na utekelezaji wa sheria NEMC Dkt. Thobbias Richard amesema awali mara baada ya Waziri kutoa maagizo walifika kufanya tathimini na kutoa maelekezo ya wawekezaji ambayo hayatekelezwa.
Ametaja miongoni mwa maelekezo ni pamoja na kutochimba na kuchenjua madini ndani ya mto na badala yake kuangalia maeneo mengine ili kutunza mazingira na uhifadhi wa Mto.
Mwekezaji wa kampuni ya G&I Seleman Kaniki amesema tangu Serikali kusitisha kuendeleza shughuli za uchimbaji amekwama kuendelea kuchangia miradi ya maendeleo ya wananchi licha ya kuchangia ujenzi wa miundombinu ya elimu, kituo cha polisi na mingineyo.
No comments:
Post a Comment