Tuesday, January 23, 2024

KT. TULIA AKABIDHI NYUMBA KWA MZEE MWENYE UHITAJI NONDE, JIJINI MBEYA.

Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) ambaye pia ni Spika wa Bunge la Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dkt. Tulia Ackson amemkabidhi nyumba ya kuishi, kitanda na godoro Mzee Aswile Mwakigege mkazi wa Kata ya Nonde Jijini Mbeya.

Nyumba hiyo imekabidhiwa  leo Jumanne Januari 23,2024 katika hafla fupi  huku ikielezwa nyumba hiyo imejengwa kupitia taasisi yake ya Tulia Trust  ambayo Dkt Tulia ni Mkurugenzi.

Hatua ya Taasisi hiyo kumjengea nyumba ,mara Mzee Aswile ni baada ya makazi aliyokuwa akiishi kubomoka na kupelekea mzee huyo kukosa makazi rasmi.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi nyumba hiyo, Dkt Tulia ameitaka jamii kuwakumbuka wazee wasiojiweza pale panapokuwa na mahitaji.

“Ndugu zangu nafanya haya kuikumbusha jamii kuwasaidia wazee wenye uhitaji tusiwaache kwani kwenye jamii zetu wako wengi wenye uhitaji sio mpaka tufike viongozi.

Wakati huohuo, Dkt. Tulia ameendelea zoezi la kukabidhi msaada wa sare za shule na madaftari kwa Wanafunzi wa shule za msingi wasiojiweza katika Jimbo hilo katika Kata zote 36.

“Tutaendelea kuwekeza kwa jamii yenye uhitaji kwa kujenga makazi bora ili kuishi kama jamii nyingine” amesema.

Akizungumza wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa nyumba hiyo, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Taasisi ya Tulia Trust, Joshua Mwakanolo amesema hiyo ni nyumba ya saba kusaidia walengwa wenye uhitaji.

“Kupitia mradi wa “Tulia mtaani kwetu” hii ni nyumba ya saba kuwasaidia wazee wasiojiweza kwani Jiji la Mbeya ni tano na Wilaya ya Rungwe ni mbili na hili ni zoezi endelevu kwa walengwa wengine wenye mahitaji” amesema.

Mkazi wa Nonde, Tabia Solomon ameishukuru Taasisi ya Tulia Trust chini ya Mkurugenzi wa Mbunge wa Mbeya mjini, Dk Tulia kwa kugusa makundi ya wazee na wenye uhitaji .

Wakati huo huo Dkt. Tulia amekagua miundombinu ya shule za msingi ya Nonde na Ilomba Jijini Mbeya na kueleza mikakati ya Serikali katika kuboresha miundombinu ya vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo.


No comments:

Post a Comment