Wednesday, April 30, 2025

DC MBARALI AMALIZA MGOGORO WA WAKULIMA, WAFUGAJI NA MWEKEZAJI SHAMBA LA NARCO MWATENGA


Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya Kanali Maulid Sulumbu amesikiliza kero Kitongoji cha Manzega Kijiji cha Kilambo Kata ya Mwatenga kuhusiana na mgogoro wa wananchi na mwekezaji David Kaaya wa Kampuni ya O.C Industrial Holdings katika shamba la NARCO.

Akifungua mkutano Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilambo Mwakani Chagu mbali ya kushukuru ujio wa Mkuu wa Wilaya huku akiwataka wananchi kuwa watulivu.

Diwani wa Kata ya Mwatenga Omary Sagutangu amesema mgogoro wa mwekezaji na wananchi umedumu kwa muda mrefu hivyo ujio wa Mkuu wa Wilaya utakuwa suluhisho kwani vikao vingi vimefanyika katika ngazi mbalimbali bila mafanikio.

Frank Sichalwe Katibu Tawala Wilaya ya Mbarali amesema ofisi yake ilipokea malalamiko kutoka kwa wananchi hivyo kutokana na uzito huo Mkuu wa Wilaya amefika kwa ajili ya kuwasililiza.

Baadhi ya malalamiko ya wananchi wamedai kupigwa pia kuporwa fedha na mazao yao na walinzi wa mwekezaji.

Katika hatua nyingine wananchi wamelalamikia utendaji kazi wa Kituo cha Polisi Igurusi kwa kutotekeleza majukumu yake ipasavyo kwani wamedai kubambikiziwa kesi.

David Kaaya Mwekezaji anayemiliki Kampuni ya O.C Industrial Holdings amekanusha tuhuma hizo dhidi ya Kampuni yake na kwamba amekaa vikao vingi na Viongozi wa Kijiji na Kata lakini hapati ushirikiano wa kutosha na baadhi yao wamekuwa wakisaidiwa na Kampuni yake.

Pia amekanusha kupora ng'ombe 108 wa wananchi bali amesema Mahakama ndiyo iliyoamuru ng'ombe wauzwe.

Baada ya kuzisikiliza pande zote Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Kanali Maulid Sulumbu ameagiza pande zote kuacha tofati zao sanjari na kuagiza wananchi kuacha kuingia maeneo ya mwekezaji huku akiwataka walinzi kuacha kutumia silaha badala yake wakutane na viongozi wa Kijiji cha Kilambo katika kipindi kisicho zidi siku saba kuanzia April 27, 2025 kuzitatua changamoto ili kurejesha mahusiano baina ya pande hizo.

Sulumbu amempongeza mwekezaji kwa kumaliza baadhi ya malalamiko ikiwa ni pamoja na kijana aliyedai kuporwa shilingi laki mbili na ishirini na walinzi pamoja na mama mmoja kurejeshewa Powetiller iliyokuwa imekamatwa.

Hata hivyo Mkuu wa Wilaya amemtaka mwekezaji kuishi vema na wananchi na kushirikiana katika shughuli za maendeleo.

Kama Mkuu wa Wilaya asingefika mapema kuutatua mgogoro huo hali ya uvunjifu wa amani ingezidi kushamiri za wananchi kujichulia sheria mkononi kwani hivi karibuni mlinzi wa mwekezaji aliuawa kwa kile kilichodaiwa kuingia na silaha Kijijini kwa ajili ya ukamataji.

No comments:

Post a Comment