Tuesday, September 10, 2024

CHUNYA KUTUMIA BIILIONI 3 UJENZI KITUO CHA MABASI

Zaidi ya Sh 3 bilioni zinatarajiwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya chenye uwezo wa kuegesha  mabasi 100 kwa siku na vibanda 400 vya biashara.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chunya Bosco Mwangine amesema Septemba 9, 2024 wakati wa hafla ya utiaji saini ujenzi wa mradi huo baina ya Halmashauri na mkandarasi mshauri wa Kampuni ya Malk Consultants LTD ambayo itajenga kwa miezi tisa.

Mwangine amesema mradi huo utakuwa na miundombinu ya huduma mbalimbali zikiwepo za kifedha  sambamba na mabanda 400 ya biashara na kuchochea fursa kubwa kwa wananchi.

Diwani Kata ya Matundasi Kimo Choga amesema ujio wa mradi huo ni maadhimio ya baraza la madiwani kutenga fedha kujenga stendi ya kisasa ili kuwaondolea hadha wananchi waliyonayo kwa sasa.

"Kama madiwani tutahakikisha tunasimamia mradi huu kuona mkandarasi anatekeleza kwa muda wa miezi tisa iliyo kwenye mkataba ikiwa ni kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan la kutaka halmashauri kutumia mapato ya ndani kujenga kituo cha mabasi".

Kwa upande wake Diwani Viti Maalumu Kata ya Makongorosi Sophia Mwanautwa amesema kitendo cha serikali kuwekeza mradi huo utafungua fursa za kiuchumi kwa wakinamama wanaobeba bidhaa kuchwani.

"Sasa tunaelekea katika Chunya tunayoitaka lengo ni kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli kwani mradi huo utahusisha huduma mbalimbali za kiuchumi ikiwepo Taasisi za kifedha" amesema Mwanautwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera amemtaka mkandarasi kwenda na wakati na sio kikwazo cha kukwamisha mradi huo.

"Natarajia mkandarasi utakwenda kwa kasi ya ujenzi wa kituo hiki cha mabasi usije kuwa chanzo cha kukwamisha na TAKUKURU futilieni ili kudhibiti upotevu wowote" amesema Homera.

No comments:

Post a Comment