Rais wa muungano wa klabu za waandishi wa habari Tanzania UTPC Deogratius Nsokolo amesema waandishi wa Habari barani Afrika wanapashwa kuwa mabalozi wa Nchi zao na kubeba jukumu la kuelimisha Umma juu ya utekelezaji wa miradi na mipango ya Serikali katika Nchi zao.
Ameyasema hayo wakati timu ya waandishi wa Habari kutoka nchi 11 za Afrika walipotembelea Mji wa kiserikali unaonendelea kujengwa Jijini Cairo nchini Misri ambapo, waandishi wameshuhudia namna Serikali ya Misri ilivyopanga na kuanza kutekeleza Mradi mkubwa wa kuhamisha makao makuu kutoka katikati ya Jiji la Cairo kwenda pembezoni mwa Jiji eneo lililopewa jina la Cairo mpya (New Administrative Capital City - ACUD).
Nsokolo amesema waandishi wana jukumu la kuuleza Umma juu ya manufaa ya miradi mikubwa inayotekelezwa katika Nchi zao na kufuatilia utekelezaji wake wakati wote ili wananchi na Dunia ijue kinachoendelea.
Aidha Tanzania pia inaendelea kutekeleza Mradi mkubwa wa ujenzi wa Mji wa kiserikari kutoka Jiji la Dar es Salaam kwenda Mtumba, Dodoma eneo ambalo tayari Wizara zinafanya kazi.
Akizungumzia Mradi huo wa Tanzania, Msemaji wa Serikali na ya Misri katika Mradi wa Cairo Mpya Bwana, Khaled El Husseiny Soliman katika mazungumzo yake na wanahabari yaliyofanyika katika Mji huo wa ACUD, Cairo amesema, anaufahamu vyema Mradi wa Mji wa kiserikali Mtumba, ambapo Misri imekuwa sehemu ya mashirikiano katika shughuli mbalimbali za Mradi huo, pamoja na kuipongeza Serikali ya Tanzania kutekeleza Mradi huo na mingine ambayo Misri inamashirikiano nayo ikiwemo Ujenzi wa Bwawa la kuzalisha Umeme la Mwl Julius Nyerere.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Mradi huo wa ACUD Bwana, Khaled Waziri Mkuu wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa amewahi kutembelea Mradi wa Cairo Mpya na kujionea shughuli zake.
Jiji la Cairo pekee lina zaidi wa watu Milioni Ishirini na mbili (22) katika jumla ya zaidi ya watu Milioni 116 walioko nchini Misri.
No comments:
Post a Comment