Thursday, December 12, 2024

WAKULIMA WATAKIWA KULIPA MADENI MSIMU 2023/24

Chama cha Msingi cha Ushirika cha Wakulima wa Tumbaku (Lualaje Amcos) kimewataka wakulima kulipa madeni kwa wakati ili kuepuka kupigwa mnada kwa mali zao ikiwepo mashamba .

Mwenyekiti wa Lualaje Amcos, Alberto Kacheza amesema leo Desemba 12, 2024 kwenye mkutano mkuu 41 wa mwaka wa kupitia taarifa mapato na matumizi hali ya uzalishaji kwa msimu huu wa kilimo.

Kacheza amesema kuna baadhi ya wakulima kwa makusudi wamekuwa wakilimbikiza madeni ya mikopo ya pembeo kwa makusudi hali inayopelekea kupata hati za mashaka

"Leo tumepitia taarifa mbalimbali sambamba na mwenendo Amcos yetu na kupendeleza masuala ya msimu wa kilimo 2024/25 katika uwekezaji wenye tija kwenye kilimo cha tumbaku na hatua za kuwachukulia wakulima wasiorejesha fedha za mikopo" amesema.

Amesema kupitia mkutano huo wakulima wamependekeza walio na madeni na kushidwa kurejesha mali zao kama mashamba yapigwe mnada kulingana na deni husika.

Amesema mbali na changamoto za malimbikizo ya madeni kwa msimu huu wamejiwekea malengo kuongeza uzalishaji kutoka kilo milioni 1.3 mpaka 1.5 kulingana na hali ya hewa.

Amesema msimu uliopita kulikuwa na changamoto katika uzalishaji uliotokana na mabadiliko ya tabia nchi na hivyo kutofikia malengo ya uzalishaji walio jiwekea.

Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Tumbaku (Mtanila Amcos) na makamu mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Tumbaku (Chutcu ), Isaya Hussen ametaka uongozi wa ushirika huo kuwa na mpango madhubuti ya ukusanyaji wa madeni.

Kuhusu suala la changamoto za upatikanaji wa mbolea ameshauri kuwepo kwa mfuko wa pembejeo wa pembejeo wa ushirika ambao utakuwa msaada mkubwa kwa wakulima na kuacha kusubiri ruzuku  kutoka serikalini.

Afisa Tarafa ya Kipembawe Kata ya Lupa, Wilaya ya Chunya, Kassim Salum amesema serikali imetoa maelekezo kwa viongozi wa Amcos kuanza kuwachukulia hatua wakulima walioshindwa kulipa madeni.

"Kuna wakulima kwa makusudi wanakwepa kulipa madeni na kutorosha maroba ya tumbaku kuuza maeneo mengine sasa hao tutawashughulikia" amesema.

Amesema ni lazima wawajibishwe kwa mali na mashamba yao kupingwa mnada kwa mujibu wa kanuni na sheria zitakavyo elekeza .

Mkulima David Moses ameomba serikali kuboresha barabara ya Lupa kwenda kijiji cha Lualaje ili kuwarahisishia kusafirisha mazao kupeleka sokoni kutokana na kukosekana kwa miundombinu rafiki.

No comments:

Post a Comment