Sunday, December 15, 2024

JAJI MWAMBEGELE "KUJIANDIKISHA KUWA MPIGA KURA ZAIDI YA MARA MOJA NI KOSA LA JINAI"

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi nchini imewaasa wananchi kujiepusha na kosa la kujiandisha zaidi ya mara moja kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na kutakiwa kujiandikisha mara moja na kwenye kituo kimoja ili kuepuka uvunjaji wa sheria.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Jacob Mwambegele katika Mkutano wa Tume na Wadau wa Uchaguzi kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura umefanyika Jijini Mbeya leo Disemba 15, 2024.

"Kujiandikisha kuwa mpiga kura zaidi ya mara moja ni kosa la jinai, 'mtu yeyote atakaeomba kuandikishwa zaidi ya mara moja atakuwa ametenda kosa la jinai na akitiwa hatiani adhabu yake ni faini isiyopungua kiasi cha shilingi laki moja na isiyozidi laki tatu au kutumikia kifungo kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili gerezani au vyote kwa pamoja" amesema Jaji Mwambegele.

Jaji Mwambegele ameongeza kuwa kadi za mpiga kura zilizotolewa mwaka 2015/2020 zenye jina la Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni halali kisheria na zitaendelea kutumika kwenye chaguzi zijazo, hivyo zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ni haliwahusu wapiga kura wenye kadi hizo na ambao kadi kadi zo hazijaharibika, kupotea au kuhama kutoka eneo moja kwenda eneo jingine.

Nae Mkurugenzi wa Uchaguzi Ramadhan Kailima amesema jumla ya wapiga kura milioni moja wanatarajiwa kuandikishwa katika vituo elfu moja mia tano arobaini na saba Mkoani Mbeya.

Kailima ameongeza kuwa baadhi ya vituo vya kujiandikisha ni Magereza ambapo wafungwa wanaotumikia kifungo cha chini ya miezi sita wataruhusiwa kujiandikisha na kupiga kura.

Akiahirisha mkutano huo mjumbe wa Tume ya Uchaguzi Dkt. Zakia Abubakary ameyashukuru makundi yote yaliyoshiriki mkutano huo sanjari na kutoa hamasa kwa wananchi kujitokeza kujiandikisha daftari la kudumu la wapiga kura na kufanya maboresho ya taarifa zao.

Baadhi ya washiriki wa mkutano huo ni pamoja na viongozi wa kidini, vyama vya siasa, asasi za kiraia, viongozi wa kimila, wahariri wa vyombo vya habari na waandishi wa habari.

Mpaka sasa zoezi la maboresho la daftari la kudumu la wapiga nchini limefanyika katika mikoa 21 wakati kwa Mkoa wa Mbeya linatarajiwa kufanyika kwa siku saba kuanzia Disemba 27, 2024 hadi Januari 2, 2025. Kauli mbiu ya zoezi hilo ni "Kujiandikisha kuwa mpiga kura ni msingi wa uchaguzi bora".

No comments:

Post a Comment