Shahidi wa sita katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe alitarajiwa kuanza kutoa ushahidi leo Jumatano Novemba 3, 2021 katika Mahakama Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
Wakili wa Serikali Mwandamizi Robert Kidando, ameiomba Mahakama iahirishe kesi mpaka kesho kwa kuwa shahidi wao amepata tatizo la kiafya.
“Shauri linakuja kwa ajili ya kusikilizwa. mpaka jana kuna shahidi ambaye tulikuwa tumepanga kuendelea naye lakini amepata tatizo la kiafya. Hivyo tunaomba ahirisho mpaka kesho tutakapoweza kuendelea. Suala hili liko nje ya uwezo wetu,” amesema Kidando.
Kwa Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Peter Kibatala wamekubaliana na ombi hilo, lakini wakitaka upande wa mashtaka kuhakikisha wanaleta shahidi.
“Kwa kufuata amri ya Mahakama ya jana sisi tulikuwa tumejiandaa lakini kwa kuwa mambo yako hivi hatuna namna ila tunaomba tu wenzetu wajitahidi kesho tarehe 4 tuweze kuendelea,” amesema Kibatala.
Jaji Joachim Tiganga ameahirisha kesi hiyo hadi Kesho Alhamisi Novemba 4, 2021.
“Kufuatia maombi ambayo yameletwa na wakili Serikali kwamba shahidi waliyekuwa wamemwandaa amefika mahali hawezi kuja kutoa ushahidi kwa sababu zilizoelezwa za kiafya na kwa kuzingatia kuwa upande wa utetezi haukupinga basi maombi haya yanakubaliwa na shauri hili linaahirishwa hadi kesho.
“Upande wa mashtaka mnakumbushwa kuanda mashahidi ili tuweze kuendelea. Washtakiwa mtaendelea kuwa chini ya uangalizi wa Magereza,” ameeleza Jaji Tiganga.
Mbowe anakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi na kupanga kutekeleza ugaidi. Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Halfan Bwire Hassan (mshtakiwa wa kwanza), Adamu Hassan Kasekwa maarufu Adamoo na Mohamed Abdillahi Ling’wenya.